WAJUMBE wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) wamemchukulia Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, fomu ya kugombea uenyekiti wa baraza hilo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).
Wajumbe hao wakiongozwa na Grace Kiwelu, Mwenyekiti wa BAWACHA mkoani Kilimanjaro wamechukua fomu hiyo leo tarehe 23 Novemba 2019, katika ofisi za Mbaraza ya Chadema, Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Kiwelu amesema wamechukua hatua hiyo, kwa kuwa BAWACHA linahitaji mchango wa Mdee, hasa katika kipindi hiki alichodai kwamba kina siasa za kibabe.
“Ni muhimu kuendelea kuwa naye kwa sababu bado tuna muhitaji, wale wanaotaka kuchukua fomu hatujawakataza chama chetu ni cha kidemokrasia. Na kila mtu ana mtu wake, na sisi wetu ni Halima. Kina mama tumeungana, tumekuchangia sh. 250,000,” amesema Kiwelu na kuongeza;
“Kwa siasa za sasa hivi za awamu ya tano zilivyo za kibabe, mwenyekiti wetu alikuwa mstari wa mbele ametuongoza na kutuwezesha kufika hapa, ni mwanamke jembe, suluru tunampenda. Mpaka sasa hatujamuona mwingine, tuliyemuona ni Halima ameonesha kwa vitendo ndio maana tumemuunga mkono.”
Halima amewashukuru wajumbe hao wa Bawacha kwa kumchukulia fomu, na kuahidi kwamba hatowaangusha kama atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa BAWACHA.
“Miaka mitano iliyopita nililazimishwa kuchukua fomu, kwa kipindi kile sikudhani kama nilikuwa tayari, na kama mnakumbuka nililia sana kipindi kile. Lakini sasa nimeshakuwa kamanda, silii kwa sababu mlinipa jukumu,kulisogeza baraza letu kutoka lilipokuwepo mpaka lilipofika sasa hivi, “ amesema Halima.
Halima anatarajia kurudisha fomu tarehe 28 Novemba mwaka huu.
Leave a comment