June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Halima Mdee achomoka mahabusu

Halima Mdee, Mbunge wa Kawe

Spread the love

HALIMA Mdee, Mbunge wa upinzani katika jimbo la Kawe, jijini Dar es Salaam amepata dhamana leo baada kukaa ndani kwa saa 24. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI ONLINE, wakili wa Mdee, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema, Hekima Mwasipu amesema, Mdee kwa sasa yupo huru.

“Baada ya kuhangaika toka jana sasa tumepata dhamana, ataripoti tarehe 26 mwezi huu,” amesema.

Mdee alishikiliwa na jeshi la polisi jana tarehe 23 Februari 2019 kwa tuhuma ya kutoa kauli za kashfa dhidi ya Rais wa Jamhuri, Dk. John Pombe Magufuli.

Mdee anadaiwa kutoa kauli ya uchochezi alipokuwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Mikocheni, tarehe 21 Februari 2019.

Amedaiwa kusema “mtu ananunua ndege badala ya vifaa vya zahanati, hii ni akili au matope.”

Awali Wakili Mwasipu alisema “Mdee alipokea wito wa kutakiwa kufika kwenye ofisi ya mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (RCO). Alitekeleza agizo hili. Alifika kituoni hapo saa 3 asubuhi.”

Hata hivyo, baada ya kuitikia wito, aliendelea kushikiliwa na polisi mpaka alipopata dhamana leo.

Mwasipu amesema, utaratibu hauruhusu mtuhumiwa kukaa mahabusu zaidi ya saa 24 “ni haki ya Mdee kupata dhamana.”

error: Content is protected !!