November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Halima James Mdee: Kutoka U-kamanda hadi Yuda Iskarioti

Spread the love

HATIMAYE safari ya kisiasa ya aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la taifa (BAWACHA), katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima James Mdee, imefika mwisho. Anaandika Isaac Kimweri, Dar es Salaam … (endelea).

Safari ya kisiasa ya Mdee ndani ya Chadema, ilifikia tamati Ijumaa iliyopita, baada ya Kamati Kuu (CC), “kuamua kwa kauli moja,” kumfutia uanachama wake.

Hitimisho la safari ya kisiasa ya Mdee, ilianzia Jumanne iliyopita, kufuatia uamuzi wake wa kubeba wenzake 18 kwenda Dodoma kwa siri na kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalum.

Alichukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa “Chadema kiko mikononi mwake” na kwamba hakuna atakayeweza kumuondoa ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, kinyume na matarajio yake, Mdee na wenzake wengine 18, waliopochikwa jina la Covid 19, akiwamo aliyekuwa mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, walivuliwa uanachama wa chama hicho.

Walituhumiwa kwa makosa ya usaliti, kuhujumu chama, kusingizia viongozi wakuu wa chama, kughushi nyaraka za chama, kujiapisha kuwa wabunge wa Chadema, “bila ridhaa ya chama na viongozi wake” na upendeleo.

Halima Mdee

Wengine waliofukuzwa, ni aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa baraza hilo (Bara), Hawa Mwaifunga; aliyekuwa naibu katibu mkuu wa baraza hilo (Bara), Jesca Kishoa na aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat.

Wapo pia, aliyekuwa mjumbe wa CC, Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo na aliyewahi kuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka.

Wengine, ni Cecilia Pareso, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Stella Siyao, Felister  Njau na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Swali kubwa ambalo baadhi ya wananchi wanajiuliza, ni hili: Mdee na wenzake, wamepata wapi ujasiri na jeuri ya kutenda yote haya? Tujadili:

 

Mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, 28 Oktoba 2020, Chadema kilisema, hakitambui matokeo ya uchaguzi huo ambayo yalimpa ushindi Rais John Pombe Magufuli.

Aidha, kupitia kikao chake cha Kamati Kuu cha mapema Novemba mwaka huu, chama hicho kikasisitiza kuwa hakitawasilisha majina ya wabunge wake wa viti maalum.

Hakikuishia hapo. Kupitia makamu mwenyekiti wake (Bara), ambaye alikuwa pia mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Tundu Antipas Lissu kikaeleza, “atakayejipeleka bungeni, atakuwa amejifukuzisha uanachama.”

Lissu alisema, “…tumekataa kuyatambua matokeo ya uchugazi huu. Tumekataa kushiriki kwenye Bunge, kwa kuwa kufanya hivyo, kutabariki uvunjifu wa demokrasia na sheria za uchaguzi. Tumepigana vita nzuri na tumepigana vizuri.”

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, Mdee alibeba wenzake na kujisalimisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai na baadaye kuapishwa kuwa mbunge wa Chadema.

Hakuna aliyetarajia hatua hii. Hakuna aliyeamini kama Mdee anaweza kwenda bungeni “kujiapisha kuwa mbunge,” bila ridhaa ya chama chake. Hakuna.

Wala hakuna aliyedhania kuwa Mdee anaweza kusaliti wenzake na Chadema aliyokuwa anaimba siku zote, kwamba atailinda na kuitetea. Hakuna.

Mdee alikuwa kada mashuhuri ndani ya Chadema. Alikuwa mmoja wa wanasiasa wachache waliojiunga na chama hicho, akiwa bado kijana mdogo, mara baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alifahamika kwa ushupavu wake wa kujenga hoja ndani ya Bunge na ndani ya chama. Alikuwa mmoja wa makada wachache waliokipigania Chadema, usiku na mchana, kwa jasho na damu.

Hivyo basi, aliamini kuwa lolote analotaka anaweza kufanya, kwa kuwa alishawahi kufanya na hakuna aliyeweza kuthubutu kumuuliza. Aligawa nafasi za uongozi ndani ya chama, aligawa ubunge na udiwani kwa kuondoa asiyemtaka na kuweka anayemtaka. Alijipa mamlaka ya kuumba na kuumbua. Hakika, Mdee alikuwa juu ya chama na katiba yake.

Ndani ya Chadema, pamoja na kwamba Mdee alikuwa bingwa wa kutengeneza makundi, fitina na usiri katika udhalimu. Lakini bado alibebwa mithili ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda wake (njiti).

Hakuna aliyeona mabaya ya Mdee. Hakuna aliyethubutu kukabiliana naye kumueleza mapungufu yake. Wachache waliojaribu kufanya hivyo, waliishia kuondoka Chadema, baada ya kuwapachika majina ya usaliti. Wengine wameweza kubaki Chadema, lakini wakiwa hawajui kesho yao.

Akisaidiwa na swahiba wake mkuu Bulaya, Mdee alitumia ukaribu wake na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuumiza wengi. Haya aliyafanya mchana kweupe kuanzia kwa mwanachama wa kawaida, hadi kwa viongozi wenzake.

Miongoni mwa wahanga wakubwa wa Mdee, ni Isaya Mwita Charles, aliyekuwa meya wa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam.

Ukienda kufanya utafiti yakinifu na bila kupepesa macho, safari ya Isaya ya kuondoka kwenye nafasi yake ya umeya, isingeweza kukamilika bila baraka za Mdee na mwenzake mmoja ambaye bado yuko Chadema.

Mara kadhaa, Mdee alimtuhumu Isaya kuwa anatumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake. Akamgombanisha na viongozi wake wa chama, wakiwamo wajumbe wa CC na Kanda ya Pwani. Akadiriki kutamka hadharani kuwa “ni bora kuongozwa na meya wa CCM, kuliko Isaya wa Chadema.”

Nakumbuka kuwa wapo baadhi ya wanachama waliowahi kuwasilisha mashitaka yao dhidi ya Mdee, kwa katibu mkuu wa chama hicho, wakimtuhumu kwa utovu wa nidhamu, uchonganishi, ugombanishi, kutengeneza makundi na ukiukwaji wa maadili ya uongozi.

Hakuna hata kesi moja iliyosikilizwa. Na siyo tu kusikilizwa, hazikuwahi hata kufikishwa kwenye vikao vya maamuzi; na au Kamati ya Maadili ya taifa.

Tukio la Mdee na wengine limedhihirisha kuwa hakuna mtu maarufu kuliko chama kwani pamoja na heshima na umaarufu aliojijengea, kwa miaka yote hiyo, leo hii Mdee ameporomoka.

Siyo yule aliyekuwa akiitwa Sauti ya Zege, siyo aliyekuwa akiitwa “Mama Yetu” – ingawa alikuwa hafanani na jina hilo. Siyo yule ambaye wananchi walidiriki kuchanga sumuni sumuni zao za vitumbua na chapati, ili aweze kutoka gerezani,

Sasa anaitwa, “Halima Mdee Msaliti.” Anaitwa mamluki. Anapachikwa kila tuhuma na kila uchafu. Ni huyu huyu Mdee, ambaye aligoma kumpa mkono aliyekuwa katibu mkuu wake, Vicenti Mashinji, baada ya kuondoka Chadema na kujiunga na CCM akimtuhumu kwa usaliti, leo anaunganishwa na wale wale aliowatuhumu usaliti.

Lakini kuna hili jingine. Hapa Chadema walipofikishwa na Mdee leo, kumetokana na tabia ya baadhi ya viongozi wake, kubagua wanachama wao, kwa kujenga makundi ya huyu mwenzetu na huyu siye.

Kwamba baadhi ya viongozi wa Chadema, walimfanya Mdee, Bulaya na wenzake, kuwa wanachama wa daraja la kwanza, huku wengine wakifanywa daraja la pili. Wakawafanya kujenga kiburi na kujiona wao ndiyo wenye Chadema.

Kwa muktadha huo, Halima Mdee na wenzake, wananjia moja tu: Kwenda mahakamani kulinda ubunge wao. Vinginevyo, watakosa vyote – Ubunge na Chadema.

Siyoni kokote ambako wa Mdee na wenzake, wanaweza kukata rufaa Baraza Kuu (BKT), kuomba kurejeshewa uwanachama wao, kutokana na kiburi na dharauwalichokionyesha mbele ya kamati kuu.

error: Content is protected !!