October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Hali tete ‘upatikanaji wa damu salama’

Mkuu wa Programu za SIKIKA, Patrick Kinemo (kulia) akiwa na Afisa wa Idara ya dawa na vifaa tiba, Scholastika Lucas

Spread the love

DAMU salama haipatikani katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), uliopo chini ya wizara ya afya na ustawi wa jamii umeshidwa kukusanya damu ya kutosha; jambo ambalo limesababisha baadhi ya vituo vya huduma, kutumia damu inayokusanywa na ndugu, familia na jamaa wa wagonjwa.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Patrick Kinemo, mkuu wa mpango wa asasi ya kiraia ya SIKIKA; taasisi inayofanya kazi ya ushawishi na utetezi wa masuala ya afya nchini.

“Hii ni hatari kiafya. Wagonjwa wanauziwa damu; jambo ambalo linaweza kusababisha maambukizi ya magojwa,” ameeleza Kinemo na kuongeza, “utafiti wetu umebaini wilaya ya Simanjiro, mahitaji ya damu salama kwa mawaka ni chupa 145, wakati mapato ni chini ya nusu ya mahitaji hayo.”

Amesema, “Mwaka 2013 walipokea chupa 74 tu, na kati ya mwezi Februari na Machi mwaka huu, hawakuwa na akiba kabisa kwa kuwa mara ya mwisho kupokea damu ilikuwa Septemba mwaka 2014.”

Hali hiyo ilionekana pia katika wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, ambapo kati ya mwezi Februari na Machi 2015, hakukuwa na akiba ya damu salama.

Amesema, “Mahitaji yao kwa mwaka ni chupa 1,400. Lakini wamekuwa wakipokea wastani wa chupa 20 kwa mwezi, ambazo ni sawa na chupa 240 tu kwa mwaka, ikiwa ni mara sita pungufu ya mahitaji yao.”

Mkoani Dar es Salaam, SIKIKA linasema, hali ni kama ilivyo katika mikoa mingine.

Kwa mfano, hospitali ya wilaya ya Temeke imekuwa ikipokea asilimia 20 ya mahitaji ya damu salama; Amana asilimia 40 na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili asilimia 50 hadi 60 ya mahitaji yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ukusanyaji wa damu bado upo chini ya mahitaji halisi ya nchi, ambayo ni kati ya chupa 400,000 hadi 450, 000 kwa mwaka. NBTS inakusanya asilimia 38 tu ya mahitaji ya damu salama nchini kwa mwaka.

Wakati hali ya upatikanaji wa damu salama ukiwa tete, kwa takribani miaka 10 bajeti ya NBTS inategemea wafadhili kutoka nje kwa zaidi ya asilimia 80. Wafadhili wakuu wa NBTS ni serikali ya Marekani, kupitia Mpango wa Dharura wa UKIMWI (PEPFAR).

Hata hivyo, Marekani na washirika wake, wamekuwa wakipunguza ufadhili wao katika eneo hilo na kwamba mwaka huu ndio utakuwa umefika kikomo.

Kinemo ametaka serikali kuiwezesha NBTS kifedha badala ya kutegemea wafadhili.

error: Content is protected !!