January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hakuna atakayezuia Panya Road

Mmoja wa washiriki wa kundi la Panya Road, Ayubu Mohamed ambaye alifariki siku ya mkesha wa mwaka mpya

Spread the love

MAPAMBANO yaliyotangazwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova dhidi ya “Panya Road” hayatafanikiwa, anaandika Pendo Omary.

Panya Road, ni genge la watoto waliochini ya miaka 18 na vijana wanaotumia silaha za jadi – visu, mawe, virungu, shoka, bisibisi, mapanga na majambia – kupora mali za wananchi jijini Dar es Salaam.

Kifo cha Ayubu kilichosababisha genge hilo kuanza kupora ikiwa ni sehemu ya kulipiza kisasi na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama, tarehe 2 Januari 2014.

[pullquote]

Wasifu wa marehemu:

Jina kamili: Ayubu Mohamed.

Umri: miaka 20.

Elimu: Darasa la nne (shule ya msingi).

Kazi: Mshirika Panya Road.

[/pullquote]

Mkakati wa polisi kupambana na genge hili, umetokana na mmoja wa wanachama wake, Ayubu Mohamed, kupigwa hadi kufa na raia “wema.”

Sababu ya kutofanikiwa, ni njia anayoitumia Kova kuangamiza genge hilo na makundi mengi yanayofanana na shughuri za kundi hilo. Njia hiyo haiendani na sababu kuibuka kwa kundi hilo.

Kitendo cha serikali cha kujitoa katika utoaji wa huduma za kijamii, hasa elimu, afya, usafiri wa majini, angani na nchi kavu, ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa maadili nchini.

Aidha, kitendo cha serikali kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza tija, kupunguza matumizi ya serikali, kuondoa ruzuku katika sekta muhimu, ikiwamo kilimo, kumepunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa wananchi kuendesha maisha yao.

Shemsha Khaji, mkazi wa Mabibo, jijini Dar es Salaam, anakiri kuwa wakati viwanda vingi vikimilikiwa na serikali, hali ya uchumi kwa wakazi wa Mabibo ilikuwa nzuri.

Ajira za viwandani zilipatikana; wenyeji walifanya kazi na kuwa na ustawi mzuri, walizaa na kuongezeka.

“Baada ya serikali kuuza viwanda hivi, hali ya umaskini imeongezeka. Vijana hawana ajira. Wazazi wameshindwa kuwasomesha, jambo ambalo limewafanya kujiunga na makundi hatarishi,” ameeleza Shamsa.

Mbali na kundi la Panya Road, kuna makundi mengine kedekede yaliyojikita jijini na ambayo yanafanya uhalifu. Miongoni mwa makundi hayo, ni Badi Face, Mwendo wa Virungu, Panya Road na Scangaga, yaliyomo Mabibo.

Kundi jingine hatari, ni lile la Mbwa Mwitu, ambalo limetangaza serikali yake katika eneo la Mbagala.

Katika eneo la Mabibo, jimboni Ubongo, ndiko ambako ni karibu kabisa na vilipo viwanda vya Urafiki UFI, FISHNET, Twiga, Chibuku, Maziwa, Ubungo Garments na Ubungo Spinnings.

Katika muktadha huo, “kazi ambayo Kova amejipa hataiweza.” Itamshinda kabla ya kuianza. Hii ni kwa sababu, makundi haya hayakuaza hivihivi. Yamezalishwa na serikali, kulelewa na serikali na kukuzwa na serikali.

error: Content is protected !!