Friday , 1 March 2024
Home Kitengo Maisha Elimu HakiElimu yakosoa sera ya Rais Magufuli
ElimuHabari za SiasaTangulizi

HakiElimu yakosoa sera ya Rais Magufuli

Wanafunzi wakiwa wamejaa darasani huku wengine wakiwa hawana madawati
Spread the love

UTAFITI wa taasisi inayoshughulikia masuala ya elimu ‘hakiElimu’ unaonesha kuwa serikali haijafikia lengo la sera ya kutoa elimu bure iliyoahidiwa mwaka 2015, anaandika Hamisi Mguta.

Katika waraka wa Elimu Namba 5, mwaka huo, serikali iliahidi kutoa elimu ya msingi bure huku wazazi wakibakizwa na gharama za matibabu kwa watoto wao, nauli, vifaa na sare za shule.

Utafiti huo ulifanywa kwa lengo la kupata maoni kuhusiana na utekelezaji wa sera hiyo, kutathmini kiwango cha fedha kilichofika shuleni na kubainisha mafanikio na upungufu wake.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, John Kalage amesema kumekuwa na upelekaji unaoridhisha katika asilimia 95 katika shule za msingi huku sekondari ikiwa na asilimia 100 lakini utafiti unaonesha pesa haitoshi.

“Hayo ni mafanikio lakini katika kuhojiana na wadau, walimu pamoja na kamati za shule na maafisa elimu, kumekuwa na kilio kuwa haitoshelezi,” amesema.

Katika kiwango cha ruzuku serikali ilipanga Sh. 10,000 kwa kila mwanafunzi wa msingi na Sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari ambapo Sh. 6,000 katika hizo zinapaswa kwenda shuleni huku Sh. 4,000 zikiangaziwa kwenye manunuzi ya vitabu, kilichopitishwa wakati huo thamani ya fedha za kitanzania ikiwa 1,000 kwa Dola.

“Hata ukichukua kwa thamani halisi ya shilingi kwa kipindi hiki inamaana ingepaswa kuwa 22,000 kwa kila mwanafunzi, kwa maana hiyo ni kwamba thamani ya pesa inayokwenda imepungua kiwango chake cha manunuzi, yaani thamani ya 10,000 ya kipindi hiko hailingani na ya 2017,” amesema.

Amesema, utafiti huo uliohusisha shule 28 za msingi na 28 za sekondari katika wilaya za Njombe, Mpwapwa, Sumbawanga, Kilosa, Korogwe, Tabora Mjini na Muleba umeonesha kuwa fedha za ruzuku zilizopelekwa mashuleni humo hazikuzingatia idadi ya wanafunzi.

Pamoja na sera hiyo kuahidiwa Kalage anasema hata baada ya kutekelezwa kwake wazazi bado wanaendelea kuchangia gharama mbalimbali za uendeshaji kwa ajili ya watoto wao kama vile kulipa walinzi, kujenga madarasa na kulipa wapishi.

“Pamoja na hayo, sera ya elimu bila malipo imechangia kiasi kikubwa kuwepo kwa ongezeko la wanafunzi kwa asilimia 43 kwa shule za msingi na 10 kwa shule za sekondari ambalo limepelekea kujaa kwa madarasa na uhaba wa walimu,” amesema.

Hata hivyo Kalage amesema serikali inapaswa kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha sera ya elimu bila malipo inaeleweka pamoja na kuongeza kwa fedha za ruzuku kulingana na gharama za maisha kupanda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mwili wa Hayati Mwinyi kuagwa leo saa 8 Uwanja wa Uhuru

Spread the loveMWILI wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi unatarajiwa kuagwa kuanza...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi kuzikwa Machi 2 visiwani Unguja

Spread the loveMWILI wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania,...

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

error: Content is protected !!