August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Haki za wanawake kuipeleka TGNP Mlima Kilimanjaro

Spread the love

 

MTANDAO wa jinsia Tanzania (TGNP-Mtandao) kwa kushirikiana na Action Aid wanatarajia kuwashirikisha wadau kupanda mlima Kilimanjaro hapo mwezi Oktoba mwaka huu ili kupaza sauti kudai haki za wanawake ikiwemo umiliki wa ardhi, anaandika Christina Haule.

Lilian Liundi, mkurugenzi mtendaji  wa TGNP-Mtandao amesema hayo katika kongamano la tamasha la jinsia ngazi ya wilaya lililofanyika kwenye kata ya Mkambarani, manispaa ya Morogoro.

Liundi amesema, “licha ya wanawake kuwa wazalishaji wakubwa lakini wamekuwa wakikosa mikopo katika taasisi za kifedha kufuatia kukosa hati miliki za ardhi jambo linalowafanya kushindwa kutekeleza mambo mengi ikiwemo kukuza mitaji yao.”

Amefafanua zaidi kuwa, kwa kupanda mlima Kilimanjaro wataweza kufikisha madai yao katika maeneo mbalimbali husika ikiwemo katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADEC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ili zitungwe sera zitakazowapa haki wanawake.

Grace Kisetu, mratibu wa harakati hizo maarugu kama Kilimanjaro Initiative, amesema, washiriki kutoka wilaya mbalimbali za mikoa 12 za Tanzania wameshiriki kongamano hilo na wamefanya tafiti katika vijiji vya wilaya ya Morogoro Vijijini na kuibua changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji duni wa huduma za afya, elimu na maji.

Kongamano hilo ni mwanzo wa harakati za kuwapigania wanawake ambapo mwezi Oktoba, mwaka huu, wanawake kutoka nchi 15 za Afrika, watakutana na kupanda mlima Kilimanjaro ili kutoa msukumo wa utekelezaji wa sera mbalimbali za wanawake.

Janeth Mawenza, mratibu wa kituo cha taarifa na maarifa kutoka Dar es salaam amesema, licha ya kuwepo haki miliki za kimila lakini katika maeneo mengi bado mila zinakwamisha wanawake kumiliki ardhi.

“Ni vyema Serikali ikaweka msisitizo katika utekelezaji wa sheria ya umiliki ardhi, na ifanye upembuzi wa kutambua wamiliki wa ardhi kwa kila kaya kwenye wilaya na kuainisha idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi ili kuweza kumkomboa mwanamke,” amesema.

error: Content is protected !!