Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao kwenye magonjwa yasiyoambukiza hususani saratani kutokana na idadi ya wagonjwa hao kuongozeka hadi kufikia wagonjwa 40,000 kila mwaka. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Jumatano tarehe 6 Aprili 2022, kwenye Chuo cha Tiba na Sayansi cha Muhimbili (Muhas) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi wakati wa mawasilisho ya tafiti mbalimbali zinazohusu saratani ya damu.

Amesema takwimu ya wananchi wanaokutwa wakiwa na maradhi ya saratani imefikia idadi ya wananchi 40,000 kila mwaka ikiwa hao ni wale ambao wamegundulika kutokana kuwa katika hali mbaya kiafya.

“Tunashauri kila mwaka au kila miezi sita kwa mwenye uwezo afanye uchunguzi wa kuangali afya yake hasa kwenye maradhi yasiyoambukiza pamoja na saratani,” amesema Profesa Makubi

Amesema dalili za saratani ziko nyingi kwa hiyo wananchi wasipuuze dalili zozote za ugonjwa au kutojisikia vizuri kiafya.

“Dalili za saratani zipo nyingi, unaweza kupungua uzito, kujisikia homa, kupungukiwa damu au kukohoa damu na matatizo ya tumbo,” amesema

Amesema kwa saratani ya tumbo, wananchi wanapojisikia hawako sawa kiafya ni vizuri kwenda kupima mapema ili kujua kama ni ugonjwa wa kawaida au ili upate uhakika kuwa ni ugonjwa wa kawaidi ni muhimu kwenda kufanya uchunguzi.

Profesa Makubi amesema wataalamu mbalimbali wamekutana Muhas kwa ajili ya kuwasilisha tafiti mbalimbali zinazohusu saratani na kwamba wanalitumia jukwa hilo juu ya kuelemisha wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa yasiyoambikiza.

Naye Ahlan Nasser, mmoja wa watafiti juu ya maradhi hayo amesema, wagonjwa wa saratani hufikishwa hospitali wakiwa kwenye hatua za mwisho ambapo ni ngumu kupata ufumbuzi wa tiba.

“Saratani ikiwa kwenye hatua ya awali inatibika hivyo natoa wito kwa Watanzania kuwahi mapema kwenye uchunguzi,” amesema Ahlan.

Kwa upande wake, Geralda Masalogo, mmoja wa wagonjwa waliowahi kuugua saratani na kwamba alipona kwa kuwa aliwahi kujifanyia uchunguzi ugonjwa huo ikiwa kwenye hatua za awali.

“Mimi ni miongoni mwa Watanznia waliowahi kupata changamoto hiyo ya saratani, kwa sasa naendelea vizuri kwa sababu niliwahi kupata matibabu mapema,” amesema Masalago.

Amesema yeye na watu wengine wamesajili taasisi itakayozinduliwa hivi karibu itajihusisha na masuala ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya saratani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *