August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gwajima azingirwa

Spread the love

NYUMBA ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima iliyopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima imezingirwa na polisi, anaandika Pendo Omary.

Hatua hiyo inachukuliwa ikiwa ni muda mchache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kupinga tuhuma za Gwajima kwa chama hicho tawala.

Mpaka sasa haijaelezwa sababu za Jeshi la Polisi kuchukua hatua ya kwenda kumsaka mchungaji huyo nyumbani kwake.

Hivi karibuni, taarifa ya Mchungaji Gwajima zilienea kwenye mitandao ya kijamii akituhumu CCM katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kugomea kumkabidhi uenyekiti wa CCM Rais John Magufuli.

Vyombo vya habari hivi karibuni vimeripoti taarifa ya kuwepo kwa mgogoro ndani ya CCM kuhusu hatua ya Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM kugoma kumkabidhi chama Dk. Magufuli.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Rais wa Nchi anayetokana na CCM ndiye anayepaswa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Kikwete anapaswa kukabidhi chama kwa Dk. Magufuli mwaka 2017.

Mbele ya waandishi wa habari leo, CCM kimepinga madai ya Mchungaji Gwajima kuhusu ‘uwepo wa kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi wakishawishi wanachama kumuunga mkono Dk. Kikwete aendelee na mwenyekiti.’

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Christopher Ole Sendeka, Msemaji wa CCM inaeleza kuwa, tarehe 11 Juni, 2016 akiwa kanisani kwake, Mchungaji Gwajima alitoa kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi dhidi ya CCM, Dk. Kikwete, Rais Magufuli, Viongozi wa CCM, Watendaji wa CCM na Serikali ya Awamu ya Nne.

“Mchungaji Gwajima amedai eti kwamba lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi wakishawishi wanachama na wakimshawishi Mwenyekiti wa sasa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ili aendelee na Uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.

“Napenda kuwafahamisha wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa, madai hayo ya Mchungaji Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na hadithi ya kufikirika.

“Watu hao hawapo kwani kama wangekuwepo habari hizo zingekwishajulikana chamani kupitia mfumo mahiri wa usalama na maadili wa ndani ya CCM,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema “kama mambo hayo yangekuwepo, viongozi wa chama wa mikoa, wilaya na matawi waliofuatwa wangekuwa ndiyo wa kwanza kuwafichua.”

Katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana, Mchungaji Gwajima aliunga mkono vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Edward Lowassa, mgombea urais kupitia Chadema ndiye aliyewakilisha umoja huo kwenye uchaguzi huo.

error: Content is protected !!