August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gwajima azidi ‘kukaangwa’ 

Spread the love

UPANDE wa Jamhuri umeendelea kupeleka mashahidi kortini katika kesi inayomkabili  Josephat Gwajima, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ya kushindwa kuhifadhi silaha yake, anaandika Faki Sosi.

Sajenti DSSGT Arobogast, shahidi wa tatu katika kesi hiyo inayounguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ametoa ushahidi wake akiongozwa na wakili wa serikali Shedracki Kimaro, mbele ya Cypriana Mkeha, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo.

Katika kesi hiyo ambayo Askofu Gwajima anadaiwa kati ya Machi 27 na 29 mwaka jana. jijini Dar es Salaam alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi tatu za pisto na risasi 17 za Shotgun, wakili wake ni mwanasheria maarufu Peter Kibatala.

Siku ya leo, Sajenti Arobogast ambaye ni mpelelezi wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, alitoa ushahidi wake kama ifuatavyo;

Wakili Kimaro: Ulikuwa wapi na nani, siku ya terehe 29 Machi, 2015?

Sajenti Arobogast: Niliitwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda maalum Costantine Massawe na nilikuwa na Inspekta Mayela.

Wakili Kimaro: Nini kilifuatia?

Sajenti Arobogast: Tuliamuriwa kwenda kituo cha Polisi cha Osterbay ambapo tuliambiwa kuna watuhumiwa walikamatwa na silaha kinyume na sheria, tulipofika kituoni hapo na kukutana na Mkuu wa upepelezi Mkoa wa Kinondoni ambaye alitukabidhi begi lenye silaha aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi tatu za pisto na risasi 17 za Shotgun, CD mbili za muziki, kitabu cha hundi ya benki ya Equity na kitabu cha Silaha , Passport ya Askofu Gwajima pamoja na Chupi.

 

Wakili Kimaro: Ieleze mahakama ikiwa kama mpelelezi uligundua nini usiku wa tarehe 29 Machi, 2015.

Sajenti Arobogast: Tuligundua kuwa mtuhumiwa namba 2, 3, na 4 usiku wa manane katika hospitali ya TMJ walikuwa na begi lenye silaha.

Wakili Kimaro: Kwa mujibu wa kazi yako kuwakuta watuhumiwa hao wakiwa na silaha usiku katika Hospitali ya TMJ inaashiria nini?

Sajenti Arobogast: Tuligundua kuwa wanamiliki sihala kinyume na sheria.

Wakili Kimaro: Washitakiwa walikaa na silaha hizo kwa muda gani.

Sajenti Arobogast: Siku mbili, tarehe 26 na 27 Machi 2015.

Wakili Kimaro: Ni utaratibu upi unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa mtu mwenye anayemilikishwa silaha?

Sajenti Arobogast: Ataelekezwa namna ya kuhifadhi silaha hiyo nyumbani kwake.

 

Wakili Kimaro: Kwa ujumla upelelezi wenu umegundua nini?

Sajenti Arobogast: tumegundua kuwa mshitakiwa namba 2, 3 na 4 walimiliki silaha kinyume na sheria na kwamba mtuhumiwa namba moja (Gwajima), alishindwa kuhifadhi silaha.

 

Baada ya wakili wa serikali kumuongoza Sajenti Arobogast kutoa ushahidi wake, Peter Kibatala wakili wa upande wa utetezi, amemuhoji shahidi huyo kama ifuatavyo;

 

Kibatala: Ulisema begi ulilolikuta na silaha lina rangi gani?

Sajenti Arobogast: Njano.

Kibatala: Lakini mbona begi lilikuwa lina rangi ya kijani, (alizungumza bila mkazo) na kuendelea; ni nani aliyechukua maelezo ya mtuhumiwa namba Moja (Gwajima)?    

Sajenti Arobogast: Mpelelezi mwenzangu.

Kibatala: Ambaye ni nani

Sajenti Arobogast: Simfahamu.

Kibatala: wakati Gwajima anahojiwa, begi lenye sihala lilikuwa wapi?

Sajenti Arobogast: Hatukuliona.

Kibatala: Mlianza kumuhoji Gwajima saa ngapi na kumaliza saa ngapi na mahojiano yaliishaje?

Sajenti Arobogast: Sikumbuki vizuri lakini tulianza majira ya saa kumi alasiri na kumaliza saa tano usiku, ambapo Mchungaji Gwajima aliugua ghafla na kuzimia.

Kibatala: Baada ya hapo nini kiliendelea.

Sajenti Arobogast: Tulimpeleka Hospitali ya Polisi ya Temeke na baadaye tukampeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili na hatimaye tukampeleka hospitali ya TMJ.

Kibatala: Ulieleza kuwa ni utaratibu wa Jeshi la Polisi kuwa ukiwa na silaha lazima utambulike. Nikisema Gwajima alikuwa anamiliki silaha kihalali nitakuwa sahihi?

Sajenti Arobogast: Ni sahihi.

Kibatala: Bila shaka  hali ya afya ya Askofu Gwajima ilikuwa sio mzuri mpaka kupelekwa katika hospitali tatu tofauti. Inawezekana alipoteza uwezo wa kuwa na maamuzi?

Sajenti Arobogast: Hapana.

Kibatala: Ni kweli kuwa mtuhumiwa namba mbili, tatu na namba nne waligundua kuwa wanamiliki begi hilo la silaha isivyo sahihi. ndio maana waliamua kulirudisha saa 8 usiku?

Sajenti Arobogast: Sahihi.

Baaada ya wakili Kibatala wa upande wa utetezi kumaliza kumuhoji shahidi Sajenti Arobogast Hakimu Mkeha ameahairisha kesi hiyo mpaka terehe 24  Novemba, mwaka huu.

Katika kesi hiyo inadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka jana jijini Dar es Salaam, Gwajima alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi tatu za pisto na risasi 17 za Shotgun.

Shitaka la pili na la tatu linawakabili washtakiwa Yekonia Bihagaze (mshtakiwa wa pili), mfanyabiashara George Mzava (mshitakiwa wa tatu) na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu (mshitakiwa wa nne) wakidaiwa kukutwa na begi lililokuwa na silaha hizo.

error: Content is protected !!