August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gwajima afyatuka, ataka Makonda ang’olewe

Josephat Gwajima, Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima

Spread the love

SIKU moja baada ya Paul Makonda kumtaja Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuwa ni miongoni mwa watu 65 wanaoshukiwa kujihusisha au kuwa na taarifa juu ya biashara ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam, hatimaye mchungaji huyo amejibu mapigo, anaandika Charles William.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Gwajima amesema Makonda ana chuki binafsi na yeye na kwamba chuki hiyo ni ya muda mrefu huku akimtaka Rais John Magufuli ambadilishie kazi kijana huyo.

“Namuomba Rais ambadilishie kazi Makonda, hii ya Ukuu wa Mkoa kutawala na kuongoza hata asiowapenda imemshinda.  Sisemi afukuzwe kazi, hapana nasema abadilishiwe kazi,” amesema.

Gwajima amedai kuwa Makonda ana chuki na wivu dhidi yake ndiyo maana alionekana kukasirika hata alipomuona Mchungaji huyo akishuka kwa helkopta yangu siku ya mechi ya viongozi wa dini na wabunge Dodoma.

“Nilichelewa kidogo nikaamua kupanda helkopta yangu mpaka uwanjani. Niliposhuka alionekana kuwa na chuki usoni dhidi yangu. Mimi nilicheza namba kumi  Makonda namba tisa,  jicho alilokuwa ananiangalia ni la chuki mpaka nikawa nashangaa.

“Makonda aliwahi kuja kanisani kwangu akiwa na marehemu sitta na akapanda mazabahuni ili nimuombee je, hakujua kama nauza unga? Hili ni shambulio kwa kanisa na sio kwa Gwajima,” amesema.

 Mchungaji Gwajima amesema kauli ya Makonda dhidi yake inaweza kusababisha watu waliookoka waonekane hawafai ndani ya jamii huku akisema kilichotokea ni shambulizi dhidi ya maaskofu na wachungaji wote.

Ameeleza kuwa kanisa lake lina waumini zaidi ya elfu sabini wanoenda kanisani kwake na katika makanisa mengine zaidi ya 400 nchi nzima na hivyo kuumuhusisha na dawa za kulevya ni kumdhalilisha.

“Makonda anafanya hivi kwa maslahi ya nani? Nani anamtuma?

“Amefanya shambulio dhidi ya Ukristo na namuomba Rais wangu mpendwa ambadilishie kazi kwani mimi namfahamu vizuri Rais,  hawezi kumtuma Makonda kufanya mambo haya,” amesema.

Amedai kuwa kijana huyo amevuka  mipaka kwa sasa. “Atakemea polisi,  atakemea jeshi, atakemea wabunge, Makonda atakemea mpaka Waziri Mkuu. Wabunge wameungana kutumia sheria na kanuni zao watamuhoji, Sisi raia wa kawaida tusio na sheria wala kanuni za kututetea tutashtaki wapi?” amehoji Gwajima.

error: Content is protected !!