August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gumzo kutoonekana kwa binti wa Obama

Sasha Obama

Spread the love

KUTOONEKANA kwa Sasha Obama, mtoto wa Rais Barack Obama anayemaliza muda wake wa kuliongoza taifa la Marekani katika mkutano wa kuwaaga raia wa nchi hiyo kumeleta minong’ono mingi, anaandika Wolfram Mwalongo.

Sasha mwenye umri wa miaka 15, mtoto wa pili wa Rais Obama hakuonekana ndani ya ukumbi wa McCormick mjini Chicago ambako kiongozi huyo alitoa hotuba kwa mara ya mwisho, akiwa amebakisha siku sita tu kabla ya kuondoka katika Ikulu ya nchi hiyo.

Imekuwa ni kawaida kwa Rais Obama kuambatana na familia yake katika matukio muhimu ya kitaifa, ambapo mkewe Michelle na watoto wake Malia walihudhuria tukio hilo huku Sasha akikosekana na hivyo kuzua maswali.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtandao wa USA Today, inasemekana kuwa Sasha hakuhudhuria mkutano huo kutokana na kukabiliwa na mitihani katika shule ya Sidwell, shule inayotajwa kuongoza kwa kufundisha watoto wa vigogo wa taifa hilo.

Katika hotuba yake ya kuaga Rais Obama alitoa hotuba iliyovuta hisia za wengi huku yeye mwenyewe pamoja na wananchi aliokuwa akiwahutubia wakitokwa machozi mara kadhaa.

Rais Obama alimuelezea mke wake Michelle kama nguzo yake muhimu kwa miaka 25 huku pia akimpongeza kwa namna alivyoifanya Ikulu ya nchi hiyo kuwa mahali pa kila mtu na hata kizazi kipya kumtazama mwanamama huyo kama mtu wa kuigwa.

Rais huyo wa 44 wa Marekani pia aliwaonya raia wa nchi hiyo kutobaguana na kushirikiana katika kuliletea maendeleo taifa hilo katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi na teknolojia.

error: Content is protected !!