June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Green guard wafunga ofisi UVCCM

Vijana wa Ulinzi wa CCM (Green Guard) wakiwa mafunzoni

Spread the love

HALI si shwari ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Magu, Mwanza (Green guard) baada ya umoja huo kufunga ofisi hizo kwa kufuli kuzuia katibu wake Kashinde Shambogo kuingia. Anaandika Moses Mseti … (endelea).

Vijana hao walifikia hatua hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa, katibu huyo ameshindwa kuwathamini licha ya kuwatumikisha katika kazi za chama hicho ikiwemo ile ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipofika wilayani hapo.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wilaya hiyo baada ya kufunga ofisi na kumzuia katibu huyo wanayemtuhumu kuchukua fedha zao za kujikimu za siku mbili zilizotolewa wakati wa mkutano wa Kinana wamesema, hawapo tayari kuendelea na kiongozi huyo.

Vijana hao zaidi ya 30 wamesema, wanamtaka Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa huo, Renatus Mhangwa aliyesimamishwa kazi na uongozi wa Mkoa kwa madai ya shinikizo la katibu huyo arejeshwe kazini.

Kiongozi wa Green Guard, Charles Ndarahwa amesema, kufunga Ofisi za UVCCM ni kushikiza uongozi wa ngazi ya juu wa chama kumchukulia hatua katibu huyo ambaye amekuwa akiwanyanyasa na kukihujuma chama kitendo ambacho kitasababisha CCM kuanguka katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. 

“Sisi hatuwezi kuendeshwa na kutumika na CCM, haiwezekani mtu apewe fedha za kujikimu halafu atukimbie na viongozi wa juu wengine tumewaambia lakini hatujasikilizwa,” amesema Ndarahwa na kuongeza kwamba;

Chama hicho hakiwezi kuendeshwa kama taasisi ya watu binafsi na kwamba, wamefikia hatua ya kufunga ofisi kwa kutumia kufuli ili kuzuia ‘uhuni na unyanyaswaji’ unaofanywa na katibu huyo.

“Huyu katibu wa vijana anataka kukiangamiza chama, mimi nadhani hana uchungu na wana Magu kutokana na kukiendesha chama hiki kwa maslahi binafsi, viongozi ambao ni wachapa kazi wanafukuzwa.

“Katibu huyu ni mzigo, anataka kukiangamiza chama chetu, anafanya haya kwa makusudi kwa kuwa anafahamu kuwa yeye muda wake unamalizika, hivyo tunaomba viongozi wa ngazi za juu kuingilia kati mgogoro huu,” amesema.

Shambogo ameliambia MwanaHALISI online kuwa, hawezi kuzungumzia suala hilo na kumtaka mwandishi kusubiri baadaye, alipopigiwa simu kwa mara ya pili, hakupatikana.

Mwenyekiti wa UVCCM Magu, Renaatus Mhangwa alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia tukio hilo amesema, ni kweli tukio hilo lipo na kwamba chanzo chake ni kusimamishwa katibu wake.

Mgangwa amesema, mara nyingi kundi hilo la ulinzi limekuwa likimlaumu katibu wake lakini utatuzi wa tukio hilo umekuwa ukisuasua.

error: Content is protected !!