Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Gombaneni lakini kunyimana hapana!  
Makala & Uchambuzi

Gombaneni lakini kunyimana hapana!  

Spread the love

NAWAKARIBISHA katika safu hii ya Jamvi la Babu Jongo. Babu yenu niko salama na pia namshukuru Muumba kwa kunijaalia afya na uwezo wa kuandika katika safu hii siku ya leo. Anaandika Babu Jongo…(endelea).

Kama kichwa cha mada ya leo kinavyosomeka “Gombaneni laki kunyimana hapana…”

Kama tujuavyo wapenzi wasomaji; kwenye wengi kuna mengi. Na wahenga walisema “Ikiwa vikombe kabatini vinagongana basi hata binaadamu wanaoishi pamoja hugongana.”

Wahenga hawakuwa na maana ya kugongana vichwa wala kupigana mateke. Bali walikuwa na maana pana zaidi katika msemo huu.

Kwamba, watu mnaoishi pamoja lazima kutakuwa na siku ‘mtapishana kauli.’ Mtagombana kwa sababu yoyote ile. Kwani sababu za kugombana zipo nyingi, inategemea tu na mtu unavyoyachukulia makosa ya mwenzio. Kwa sabau hakuna mkamilifu. Yaani hakuna asiyekosea. Hayupo.

Sasa inapotokea kutoelewana kati yenu, msifike mbali katika kutoa uamuzi. Kuweni wepesi katika kusameheana na kusahau kosa. Nasema hivi kwa makusudi kabisa, kuna watu wengine wepesi kusamehe mdomoni lakini wanabakisha moyoni. Hii haipendezi.

Kama umeamua kumsamehe mwenzio basi fanya hivyo, kwa moyo mkunjufu, ukiliweka moyoni kosa la mwenzio hutamtendea haki. Ni wazi kwamba kuna haki zake za msingi utakazo mnyima, jambo ambalo halifai.

Gombaneni lakini linapokuja suala la haki za msingi msinyimane. Kuna wakati wanandoa wakiudhiana hulipizana kwa kutopeana huduma.

Mwanaume hukatisha huduma anazozitoa kwa mkewe kama matumizi na huduma nyingine na mke naye hukatisha huduma anazozitoa kwa mume, wakati mwingine hugoma hata kupika na huduma muhimu ya unyumba.

Najua mtu ukikosewa utataka kuonyesha hisia zako kutokana na kosa ulilotendewa, lakini kama utafanya hivyo ujue wazi kuwa unafanya makosa. Mumeo au mkeo amefanya kosa na wewe unafanya kosa. Kosa halilipwi kwa kosa.

Mchana kutwa ulimnunia mwenzio. Tayari adhabu tosha hiyo! Lakini huridhiki unataka kuongeza adhabu nyingine – tena kubwa zaidi. Unamnunia mwenzio mpaka kitandani! Hii haikubaliki.

Kununiana mpaka vitandani haifai, huko ni kupanda mbegu ya sumu ambayo wavunaji wake ni ninyi wenyewe. Itaua ndoa yenu mngali mnaipenda.

Katika kadhia hii wanawake wanaongoza. Akili zao zinawatuma kuwavalia kaptura za majinzi waume zao ndio njia sahihi za kuwakomoa.

Hapana ndugu zangu; hiyo sio njia sahihi ya kumhukumu mwenzio. Wakati mwingine wanaume wanatumia kisingizo hicho cha kunyimwa unyumba kwa kujivinjari na ‘vichenchede.’ Wenyewe wanasema huko ni “kumsusia nguruwe shamba la miwa kama sio kumpiga teke chura.”

Sina maana wanawake peke yao wenye tabia hizo. Wapo wanaume wengi wanaowanyima hata matumizi wake zao baada ya kugombana. Eti anataka kumkomoa. Dume kama hili halijui kama kumnyima matumizi mkewe hakumkomoi mke pake yake, hata yeye atakomoka.

Ndiyo; si atajirahisisha kwa ‘Babu Jongo’ ili apate mahitaji. Sasa nani atakomoka zaidi? Kwetu tunaita “hasira za mkizi faida kwa mvuvi.” Kama kulikuwa na jamaa anayemnyemelea mkeo ndio unampa nafasi hivyo!

Wanandoa mnatakiwa kupunguza visasi, kinyme cha hivyo mtakuwa mnakaribisha adui katika ndoa yenu. Kumbukeni msemo wa “ukimpata mng’ang’anie.” Mdhibiti asije akakutoka maana wewe ukisema wanini wenzio wanamtolea macho na kusema watampata lini.

Chonde wanandoa mnapogombana jaribuni kuyasawazisha matatizo yenu haraka kabla ‘shetani’ mmbaya hajachukua nafasi. Tendo la ndoa ni kama chakula, ukimyima wewe atatafuta pakulipata ili ale. Sio rahisi kukaa kusubiri njaa imuumize.

Uzuri wa tendo la ndoa wakati mwingine linakuwa kisuluhisi cha ugomvi. Hata kama mmenuniana mchana kutwa, lakini usiku ukaruhusu kumpa naye akakupa mtajikuta ugomvi unaishia hapo. Mkitoka hapo ugomvi kwisha kabisaaa. Jaribu uone.

Gombaneni laki kunyimana hapana jamani!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake

Spread the loveBUNGE la Jamhuri linaloendelea mjini Dodoma, kwa wiki nzima limetawaliwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Wamesahau aliyofanya Magufuli

Spread the loveJUMATATU ya tarehe 16 Oktoba 2023 itabaki kuwa siku ya...

error: Content is protected !!