January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

GMS: Ninashangaa wanaonihujumu wanalindwa

Waziri Lazaro Nyalandu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu

Spread the love

KAMPUNI ya Green Mile Safari (GMS) ambayo imefutiwa leseni ya uwindaji kwa madai ya kuvunja sheria ya uwindaji ya mwaka 200, inadai uamuzi huo unahitimisha mpango wa muda mrefu wa kumzuia kuendeleza vitalu alivyopewa, kwa sababu ya “wivu tu wa kibiashara.”

Aidha, inahoji kwamba iweje washushiwe tuhuma na kuadhibiwa bila ya kuelezwa makosa yao huku ikijulikana wazi kuwa waliajiri mtaalamu wa uwindaji kwa ajili ya kusimamia safari ya wageni wao; mtaalamu ambaye hajachukuliwa hatua yoyote.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Awadh Ally Abdallah ameiambia MwanaHALISI Online kwamba wakati anapewa adhabu kupitia vyombo vya habari Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ameendelea “kujizuia” isivyoeleweka kuwaondoa washindani wake kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited (WWS).

“Mimi ninayefanya shughuli zangu kwa shida kutokana na vikwazo nilivyowekewa na mshindani, kinyume cha sheria, ninaadhibiwa. Yule ambaye anatufanyia fujo na kuikosesha mapato serikali, ambaye ilishaelekezwa aondolewe kwa nguvu, analindwa na Waziri. Inasikitisha sana,” amesema.

Awadh amesema Waziri Nyalandu anajua vizuri mezani kwake tangu Mei mwaka jana, alishauriwa na wataalamu wa Idara ya Wanyamapori kumuondoa WWS kwa kung’ang’ania kitalu isivyo halali kisheria, lakini hajachukua hatua yoyote.

“Tulikuwa na professional hunter tuliyemwajiri maalum ili kuongoza safari ya wageni wetu kuwinda mwaka 2012. Jukumu lake ni pamoja na kusimamia uwindaji usioharibu wanyama na mazingira yao,” alisema.

Awadh alisema “wageni wetu hawakuwa peke yao. Walikuwepo maofisa wa wanyamapori ambao wamesomea kazi pamoja na walinzi pia walikuwepo. Wote hawa walikuwa wapi wakati makosa yanayodaiwa kufanywa yalipokuwa yakitendwa.

“Sisi tunasikitika kutangaziwa adhabu hewani kama vile tupo mbali na Wizara. Hatujajulishwa lolote ili nasi tutoe maelezo yetu. Hakuna mawasiliano yoyote tuliyoyapata kutoka Wizara ya Maliasili,” alisema kwa mshangao.

“Hadi sasa hatujafahamishwa rasmi hicho kinachotajwa na vyombo vya habari kuwa tumekitenda. Inakuaje mtu anapewa adhabu bila ya kujulishwa kosa lake,” anahoji.

“Baada ya kusikia tunavyotuhumiwa, niliomba maelezo ya tuhuma kwa sababu mimi sina uwezo wa kuingia bungeni na kusema pale ninapotuhumiwa. Sijajibiwa kitu hadi leo… wananichukulia hatua kali pasina kunipa nafasi ya kujitetea. Hizi sheria katili hivi zinatoka wapi jamani,” amesema.

Awadh anasema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda kumuomba ufafanuzi wa tuhuma dhidi yake ambazo zilitolewa bungeni na Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa.

Hata hivyo, Awadh anashangaa kutojibiwa lolote mpaka sasa hali inayothibitisha kuwepo mpango wa kumchafua bila ya kupewa nafasi ya kujitetea.

Julai 11, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alitangaza kufuta leseni ya kuendesha vitalu vya uwindaji ya kampuni ya GMS kwa maelezo kuwa imevunja sheria ya uwindaji.

Siku mbili baadaye, GMS kupitia kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, imesema hatua hiyo ni kutekeleza matakwa ya washindani wao kampuni ya Wengert Windrose Safaris (WWS) ambayo imekuwa ikiwania kitalu kilichomilikishwa kwa GMS mwaka 2013.

error: Content is protected !!