August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Giza latanda kutoweka kwa Ben Saanane

Bernard Saanane, Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Spread the love

BERNARD Saanane, Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hajulikani alipo kwa zaidi ya wiki mbili sasa, anaandika Charles William.

Ben ambaye amekuwa akiongoza kampeni ya ‘kumvaa’ Rais John Magufuli katika mitandao ya kijamii na hata magazetini, akihoji uhalali wa elimu yake hususan shahada yake ya uzamivu (PhD), aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hajaonekana nyumbani kwake wala kazini kwake kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

“Tumepata hofu kubwa, hatujui alipo, tumeambiwa hajafika nyumbani kwake eneo la Tabata kwa muda wa wiki mbili  na hii inaenda wiki ya tatu sasa, tumeenda kazini kwake (Makao Makuu ya Chadema), napo hawajui alipo. Namba zake zote hazipatikani,” ameeleza Agripina Saanane, dada wa Ben.

Akizungumzia namna walivyopata taarifa za kutoonekana kwa Ben Saanane, amesema familia yao ilijulishwa na mtu  anayeishi na Ben maeneo ya Tabata, jijini Dar es Salaam kuwa kijana huyo, hajaonekana kwa muda na kwamba si kawaida yake kutoonekana bila kuaga.

“Tulipopigiwa simu na kuambiwa kuwa Ben hajaonekana nyumbani kwake hatukuwa na wasiwasi sana kwasababu yeye ni mwanaharakati na mwanasiasa, tukajua huenda akawa safarini katika shughuli za chama (Chadema), hata hivyo tulipata hofu baada ya kuona siku zinapita na namba zake hazipatikani,” ameeleza Agripina.

Agripina amesema tayari familia yao ilishatoa taarifa za awali katika kituo cha polisi Tabata, ambapo walielekezwa kujaribu kuulizia taarifa za ndugu yao katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitalini wakati polisi wakifanya uchunguzi wa suala hilo.

Hapo awali, MwanaHALISI Online iliwasiliana na Tumaini Makene, ofisa habari wa Chadema taifa ili kujua ukweli wa taarifa za kupotea kwa mtumishi huyo wa makao makuu ya chama hicho, hata hivyo alishauri mwandishi wa habari hizi awasiliane na familia yake kwanza kabla ya kupata kauli ya chama.

Alipotafutwa baadaye hakuweza kupokea simu, huku Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema akimueleza mwandishi wa habari hii kuwa, “nipo kwenye kikao, naomba unitafute baadaye kidogo.”

MwanaHALISI Online pia imewasiliana na Kamishina Simon Sirro, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ili kujua kama  jeshi hilo linazo taarifa za kutoweka au kutoonekana kwa mwanasiasa huyo kijana. Simu ya Kamanda Sirro ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kama msaidizi wake huku akisema “Kamanda yupo kwenye kikao kwa sasa, mtafute baadaye.”

Itakumbukwa kuwa, leo mchana familia ya Bernard Saanane kupitia baba yake, mzee Focus Saanane ilitoa taarifa katika mitandao ya kijamii, ikieleza kupotea kwa kijana huyo kwa karibu wiki tatu sasa na kuomba msaada kwa mtanzania yoyote mwenye taarifa za mahali alipo.

Kumbukumbu katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook zinaonesha kuwa Ben aliandika kwa mara ya mwisho tarehe 15 Novemba, 2016 muda wa saa 6:45 mchana, ambapo katika andiko lake la siku hiyo alimuelezea Rais Magufuli kama mtu jasiri, lakini akibeza kuwa ujasiri huo umekuwa ukionekana zaidi katika mambo yasiyo na tija.

Kama ilivyo kawaida yake, alimalizia andiko lake hilo kwa kumtaka Rais Magufuli ahakiki shahada yake ya uzamivu- PhD na aweke wazi malipo ya mshahara wake huku akihitimisha kwa kibwagizo “A Luta Continua, Victory Ascerta” akimaanisha “Mapambano yanaendelea na ushindi upo dhahiri.”

error: Content is protected !!