July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ghasia za wafuasi wa Zuma zatishia usalama wagonjwa Covid-19

Spread the love

 

USALAMA wa maisha ya wagonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19), Afrika Kusini, uko rehani kufuatia ghasia zinazofanywa na wafuasi wa Rais Mstaafu wa nchi hiyo, Jacob Zuma. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).

Ghasia hizo ziliibuka wiki iliyopita, kufuatia hatua ya Zuma kujisalimisha gerezani, kwa ajili ya kutumikia kifungo cha miezi 15, adhabu aliyopewa baada ya kukutwa na hatia katika kosa la kudharau wito wa Mahakama ya Kikatiba ya Afrika Kusini.

Zuma alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kutohudhuria katika kesi ya ufisadi inayomkabili.

Ghasia hizo zimepoteza maisha ya watu zaidi ya 70 na kuharibu mali za wafanyabiashara, tangu ziibuke tarehe 8 Julai 2021, Zuma alipojisalimisha gerezani. Serikali ya Afrika Kusini imeingiza jeshi mtaani kudhibiti ghasia hizo.

Mapema leo Jumatano, tarehe 14 Julai 2021, Mtandao wa Kitaifa wa Hospitali Afrika Kusini (NHN), umesema hospitali zilizoko katika Mikoa ya Gauteng na KwaZulu-Natal, zinakabiliwa na ukata wa vifaa tiba, hasa mashine za kupumulia za oksijeni na dawa.

Jacob Zuma

Hospitali hizo zinakabiliwa na ukata wa vifaa tiba na dawa, kutokana na machafuko hayo, yaliyosababisha usafirishaji wa bidhaa kukwama baada ya wafuasi hao wa Zuma kufunga barabara.

Katika taarifa yake, NHN imesema, ukata wa vifaa tiba na dawa hasa mashine za oksijeni, unatishia usalama wa wagonjwa hususan wa Covid-19, ambao hupumua kwa msaada wa mashine hizo.

Mbali na ukata wa vifaa, watumishi wa hospitali hizo wanadaiwa kushindwa kufika katika vituo vya kazi, kutokana na ghasia hizo.

Kwa mujibu wa mitandao ya kimataifa, baadhi ya mikoa inakabiliwa na uhaba wa huduma muhimu, hasa ya chakula na mafuta ya petroli na dizeli.

Wafuasi wa Jacob Zuma

Vituo vya kuuzia mafuta nchini humo, vimepunguza kiwango cha uuzaji mafuta hayo, kutokana na usafirishwaji wake kuathiriwa na ghasia hizo.

Shughuli za utoaji huduma nchini humo zimeathirika, baada ya wafuasi hao kuvamia na kuchoma baadhi ya maduka na majengo.

Zuma aliyeiongoza Afrika Kusini kuanzia 2009 hadi 2018, anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na rushwa, makosa anayodaiwa kufanya akiwa madarakani.

error: Content is protected !!