June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ghasia azindua mafunzo mabasi ya mwendo kasi

Spread the love

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia amewataka madereva wanaofanyiwa mafunzo ya kutumia mabasi yaendayo kasi kuyazingatia ili kuwa na ufanisi mzuri wa kazi. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Amesema hayo katika uzinduzi wa mafunzo ya uongozaji wa mabasi yaendayo kasi chini ya Kampuni ya UDART kwa madereva uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Ghasia amesema katika kipindi hiki cha mafunzo ya utumiaji wa mabasi ya haraka, hakutakuwa na mfumo kamili wa matumizi uliopangwa kutumika katika mabasi hayo na kwamba, kutakuwa na kamera ndani ya mabasi hayo zitakazoweza kuonesha kinachoendelea ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za dharura.

Aidha amewataka watakaofanya kazi ya kuhudumia abiria ndani ya mabasi hayo kuwa wakarimu kwa abiria ili wafike katika vituo vyao kwa usalama na furaha zaidi.

“Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika ikiongozwa na Afrika Kusini kutumia mabasi yaendayo haraka na tunatarajia kuwa na mafaniko zaidi ya Afrika Kusini.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi kuzingatia na kusimamia miundombinu ya mabasi hayo kuepuka kuchakaa mapema.

Amesema mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba watu hadi 500,000 kwa nusu saa yatafanyiwa mafunzo kwa madereva chini ya uongozi wa VETA (Chang’ombe) ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi.

Mwakilishi kutoka VETA, Samwel Nganya amesema madereva watakaoendesha mabasi hayo ni wale watakapewa leseni za kimataifa na watakuwa na uwezo wa kufanya kila kitu peke yao pasipo na konda kwani mabasi hayo yanaongozwa na dereva tu.

Nganya ameongeza kuwa, madereva wanaohitajika ni 330 lakini madereva 149 ndio waliopatikana kwa majaribio ya vitendo, hivyo bado kuna uhitaji wa madereva 181 zaidi kufikia idadi kamili.

Licha ya kuwapa mafunzo madereva hao Nganya amesema, wana mpango wa kutoa mafunzo mahususi hasa kwa wahudumu wa wateja (customer care) kuhakikisha huduma zinakwenda sawa.

error: Content is protected !!