July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ghasia awabana wakurugenzi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia

Spread the love

WAKURUGENZI wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao wamerudishiwa fomu maalum za madai ya walimu ili wazifanyie marekebisho, wametakiwa kufanya haraka ili madai hayo yaweze kulipwa. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Agizo hilo limetolewa leo bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba (CCM).

Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kulipa madeni ya walimu.

Akijibu swali hilo, Ghasia alisema madai hayo ya walimu 3,356 yenye kiwango cha Sh. bilioni 3.7 yaliyowasilishwa kwa kutumia fomu maalum, yalirudishwa kwa Mamlaka za Ajira za Walimu hao ili yafanyiwe marekebisho stahiki na kuwasilishwa tena ili yalipwe.

“Wakurugenzi naomba mzishughulikie fomu hizo haraka iwezekanavyo ili madai haya yaweze kulipwa Julai 2015,”amesema.

Aidha, Ghasia amesema madai ya malimbikizo ya mishahara ya walimu 150 yenye kiwango cha Sh.milioni 284.9 tayari yameingizwa kwenye Mfumo wa Malipo ya Mishahara kwa ajili ya kulipwa kupitia orodha ya malipo ya mishahara ya Juni, 2015.

Amefafanua kuwa, madai yasiyo ya mishahara yaliyowasilishwa yalikuwa ni Sh. bilioni 5.6 ambapo kati ya fedha hizo Sh. bilioni 5.3 zimelipwa kwa walimu walio chini ya Tamisemi na Sh. milioni 286.9 zimelipwa kwa walimu na wakufunzi walio chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Ameongeza kuwa madai mengine Sh. bilioni 10.5 kutoka Tamisemi na Sh. bilioni 1.5 kutoka Wizara ya Elimu yalikataliwa baada ya kubainika kuwa baadhi yao tayari wameshalipwa na mengine yalikosa vielelezo vya kuthibitisha uhalali wake.

error: Content is protected !!