June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

GGM kuchelewesha fidia kwamkwaza Pendeza

Spread the love

PENDO Pendeza, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) ameitaka serikali kutoa maelezo ni lini itawalipa fidia wananchi wa Geita ambao walipisha mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM), anaandika Dany Tinason.

Amesema wapo wananchi ambao walipisha mgodi huo lakini hawajalipwa fidia zao hadi sasa jambo ambalo linaonekana kufumbiwa macho na serikali.

Mbali na hilo amesema, bado kuna utata mwingi katika ulipaji wa fidia katika migodi mbalimbali ukiwemo sehemu za Nyalugusu jambo linalosababisha wananchi hao kutaabika kila siku.

Awali katika swali la msingi la Deogratias Ngalawa, Mbunge wa Ludewa (CCM) alitaka kujua wananchi waliochangia ardhi ya yao kupitisha miradi watalipwa fidia lini.

Pia alitaka kujua miradi ya mkaa wa mawe wa Mchuchuma na Liganga kwamba, itaanza lini?

Akijibu swali hilo Dk.Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini amesema, wale wote ambao wanapisha maeneo yao kwa ajili ya kupisha shughuli za maendeleo, hufanyiwa tathimini na kisha hulipwa fidia.

Akizungumzia wale ambao wanatakiwa kuondoka katika maeneo ya migodi amesema, migodi huwajibika moja kwa moja kuwalipa fidia na pale muhusika asiporidhika huweza kufuata taratibu za kisheria.

Akizungumzia miradi ya Mkaa wa Mawe wa Mchuchuma na Chuma cha Liganga amesema, inasimaniwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Amesema miradi hiyo inaendelezwa kwa pamoja kati ya NDC lenye asilimia 20 ya hisa na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Company Limited ya China yenye hisa asilimia 80 kupitia kampuni ya ubia ya Tanzania.

error: Content is protected !!