January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gazeti la Uhuru lijiandae kufungiwa

Spread the love

ANGALAU gazeti moja lililofungiwa na serikali – Mwananchi – limemaliza kutumikia adhabu liliyotwishwa. Nalo gazeti la Mtanzania linatarajia kumaliza kifungo chake 26 Desemba 2013.

Lakini MwanaHALISI, gazeti la wananchi, limeamriwa na wenye nguvu kufungiwa kwa muda usiojulikana; tendo ambalo limelenga kuua wafanyakazi, watendaji wa kampuni, wasambazaji na watu wengine wanaotegemea gazeti hili kwa ujira na kuendesha maisha yao.

Wote hawa, serikali imeamua kuweka maisha yao kiganjani mwake – kuwaamulia uhai au kifo. Hii ni hatari.

Huu ndio ufedhuli wa sheria katili ya magazeti ya mwaka 1976, ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali ilisema, zaidi ya miaka 20 iliyopita, kwamba ama ifutwe kabisa au ifanyiwe marekebisho makubwa.

Sheria inatoa mamlaka kwa waziri wa habari kufungia chombo cha habari wakati wowote. Halazimishwi kukwambia mapema wala kukueleza sababu.

Tendo la serikali la kufungia vyombo vya habari, licha ya kuwa la maangamizi kibiashara; linatishia uhai wa wafanyakazi na familia zao.

Bali, ukifuatilia kwa makini vitendo hivi vyenye lengo la kunyamazisha wananchi; kuwanyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana, utabaini yote haya yanafanywa na kusimamiwa na genge la watu wachache serikalini.

Wanatenda haya siyo kwa mujibu wa sheria, taratibu na misingi ya utawala bora. Hapana. Ni binafsi. Sababu ni hizi:

Kwanza, mara baada ya gazeti la Mtanzania kufungiwa kwa siku 90, wamiliki wake waliamua kubadilisha gazeti la RAI. Badala ya kutoka kila Alhamisi, walitaka litoke kila siku.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), kwa sababu binafsi, akaamuru RAI kutochapishwa kila siku. Akaagiza gazeti liendelee kutoka kila Alhamisi.

Kisingizio cha kuzuia RAI lisichapishwe kila siku ni madai kuwa barua ya serikali ya 22 Desemba 1994, iliyotoa ruhusa gazeti kuchapishwa kila siku, ilitolewa kwa kampuni ya Habari Corporation Ltd.

Barua ya kutaka kutambuliwa leseni ya mwaka 1994, imewasilishwa kwake na kampuni ya New Habari Corporation (2006) Ltd.

Haya, kwa maelezo yake, ni kampuni mbili tofauti. Lakini mkurugenzi wa Maelezo anajua – hata kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo – kampuni ya Habari Corporation Ltd., imeuzwa kwa inayoitwa, “New Habari (2006) Ltd.”

Magazeti ya RAI, Bingwa, Mtanzania, The African na Dimba, yaliyokuwa yakimilikiwa na Habari Corporation Limited, sasa yanachapishwa na New Habari (2006) Ltd. Hili wala halifanyiki kwa siri. Ukurasa wa mwisho wa magazeti hayo unataja mchapishaji.

Aidha, sheria ya magazeti haielekezi – Msajili wa Magazeti – kutoa leseni kwa anayetaka kuuza kampuni yake. Kazi ya kubadilisha mmiliki wa kampuni, ni kazi inayofanywa na Wakala wa Serikali wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA).

Huko ndiko taarifa zote za kampuni juu ya mauziano ya hisa, usajili, kubadilisha wanahisa, wakurugenzi, wanachama, anuani, mali na madeni, zinakohifadhiwa au kuthibitishwa.

Hatua ya mkurugenzi wa Maelezo kujitwisha jukumu la msajili wa makampuni, ni kujichosha. Ni kufanya kazi isiyomhusu. Ni mkakati wa kutaka kuzuia gazeti lisichapwe. Ni suala binafsi.

Hoja kuwa barua ilitolewa kwa Habari Corporation Ltd., na siyo New Habari, haina mashiko. Gazeti lililoruhusiwa kutolewa kila siku, bado ni lilelile – RAI. Kuendelea kung’ang’ania madai kuwa mabadiliko ya kampuni yameathiri ruhusa iliyotolewa, kunaweza kuibuka madai mapya.

Kwa mfano, RAI wanaweza kusema, barua iliyotolewa na Maelezo mwaka 1994, haihusu Maelezo hii ya sasa. Maelezo ya wakati ule ilikuwa chini ya ofisi ya waziri mkuu. Maelezo ya sasa iko moja kwa moja kwenye wizara ya habari; na hivyo haina mamlaka ya kuzuia ruhusa ambayo haikutolewa na yeye.

Pili, tamko la Maelezo kutuhumu RAI kutenda kinyume cha sheria, lilitolewa tarehe 10 Oktoba 2013 – siku sita baada ya gazeti kuanza kuchapishwa kila siku na kusambazwa. Gazeti la RAI lilianza kutolewa kila siku, tarehe 6 Oktoba 2013.

Kabla ya wamiliki wa RAI kuchapisha gazeti lao kila siku, walitoa matangazo kwenye radio na televisheni. Kila gazeti lilipochapishwa lilipelekwa Maelezo kama sheria inavyoelekeza.

Kwa muda wa siku sita, Maelezo haikuona gazeti wala matangazo yanayoelekeza wasomaji wa gazeti hilo, kuwa chombo chao kiko mtaani? Hakika, waliona.

Lakini kwa kuwa ni suala binafsi, waliamua kunyamaza. Hawakuandikia wamiliki barua ya kuzuia; wala kuwaita wamiliki; na au mchapishaji.

Tatu, serikali ilituhumu kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL), “kuendelea kuchapisha gazeti lake katika mtandao kinyume na agizo la kufungiwa.”

Mkurugenzi wa Maelezo anajua hakuna popote ambako tangazo la serikali la kufungia magazeti haya – MwanaHALISI, Mwananchi na Mtanzania – kulikoelekeza kutochapisha gazeti kwenye mtandao. Hakuna.

Hii ni kwa sababu, sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inayotumiwa kuhalalisha kifungo hiki haramu, haina kifungu kinachozuia “uchapishwaji kwenye mtandao wa intaneti – online.”

Maelezo wamekiri hili la kutokuwapo sheria. Naibu msajili wa magazeti amesema kwenye mkutano ulioitishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makalla, “…hakuna sheria yeyote inayozuia gazeti kuwa online.”

Mkutano ambamo naibu msajili ameeleza hakuna sheria inayozuia online, uliitishwa na Makalla. Ulihudhuriwa na  ofisi ya msajili na wamiliki wa magazeti ya Mtanzania na Mwananchi.

Msajili ambaye amehudhuria mkutano uliokiri kutokuwapo sheria ya kuzuia online, ndiye huyohuyo aliyezuia Mwananchi kuchapishwa kwenye mtandao.

Sasa sheria iko wapi hapo? Uadilifu uko wapi? Ukweli uko wapi? Je, tukisema haya ni mambo binafsi, tutakuwa tunakosea wapi?

Au ni kweli kwamba madai ya msajili wa magazeti yalisukumwa na azimio la kutoandikwa, kutotangazwa na kutopigwa picha, kwa muda usiojulikana, lililotolewa na vyama vya waandishi wa habari, wamiliki na wachapishaji; na ambalo limejumuisha yeye na waziri wake?

Nne, hata uwiano wa makosa haulingani na adhabu. Kwa mfano, gazeti la Mtanzania lililotuhumiwa kwa kosa moja – na ambalo tayari lilishaomba radhi kwenye ukurasa wa mbele – limefungiwa kwa siku 90. Tuhuma moja siku 90.

Gazeti la Mwananchi ambalo limetuhumiwa kwa makosa mawili, limefungiwa kwa siku 14. Gazeti lililofungiwa kwa siku 14 limetumikia adhabu siku 12 tu. Hakuna anayeeleza sababu za gazeti kutumikia adhabu kinyume na ilivyoamuriwa.

Wala hakuna anayemchukulia hatua (mkurugenzi wa Maelezo) aliyetoa tangazo la kufungia magazeti hayo Jumamosi na kusema adhabu zimeanza jana (Ijumaa).

Aidha, MwanaHALISI ambalo makosa yake hayakuelezwa wakati huo na hayajaelezwa hadi sasa, limefungiwa kwa muda usiojulikana. Usawa uko wapi? Sheria iko wapi? Uadilifu uko wapi? Ni suala binafsi.

Ndiyo sababu, wahusika walishupalia kuzuia Mwananchi online, wakati wanakiri hakuna sheria ya kuzuia hilo. Kama siyo ushupavu wa Naibu Waziri Makalla, kusimamia maneno yake, gazeti la RAI lisingetoka.

Ubinafsi ndiyo unaozuia gazeti la MSETO – gazeti dada na MwanaHALISI kubadilishwa, kutoka kuandika habari za michezo na burudani peke yake na kuwa la habari mchanganyiko.

Taarifa zinasema, leo ni miezi 15 na siku tatu, tangu wamiliki wa MSETO wawasilishe taarifa kwa mkurugenzi wa Maelezo kuhusu gazeti hilo kuanza kuandika habari mchanganyiko. Hakuna aliyewajibu.

Pale mmiliki alipoanza kuandika habari mchanganyiko kwa kuamimi taarifa aliyowasilisha kwa msajili wa magazeti imejitosheleza, alipokea karipio kali la maandishi.

Karipio la Maelezo liliwasilishwa ofisini kwa mchapishaji, ndani ya saa mbili baada ya gazeti kusambazwa.

Kama ilivyokuwa kwenye online, mkurugenzi wa Maelezo hana mamlaka ya kuamuru gazeti lichape nini. Sheria inataka mchapishaji kutoa taarifa ya mabadiliko ya siku ya kutoa gazeti, sura ya gazeti na mabadiliko ya sera ofisini kwa msajili. Basi!

Kama hili siyo jambo binafsi, kipi kilichosababisha Maelezo kutojibu taarifa ya kubadilishwa MSETO; kunyamazia kwa muda wa siku sita, gazeti wanalodai limezuiwa kuchapishwa (RAI) na kuacha Mwananchi online ikifanyakazi wakati gazeti limefungiwa?

Ni kwa sababu, baadhi ya watu wanaoendesha vitendo hivi vya kufungia magazeti, wanataka kuaminisha umma kuwa wao ni wazalendo katika taifa hili kuliko wengine. Hii siyo sahihi.

Wengi wanaohaha kuhakikisha MwanaHALISI halirudi mtaani, ni wale ambao gazeti hilo limewataja kuhusika na ufisadi au vitendo vingine vya uvunjifu wa haki za binadamu. Wanafahamika.

Baadhi yao, ni marafiki wa waliopo madarakani na wenye mamlaka ya kuamuru gazeti kufungwa. Wengine ni viongozi wa vyombo vya dola walioshindwa kuzuia au wamenyamazia wizi wa fedha za umma ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT).

Wengine wameshiriki au wamenyamazia kumwagiwa tindikali kwa mkurugenzi wa gazeti hili, Saed Kubenea, kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven Ulimboka na raia wengine wa kawaida. Hawa hawawezi kuwa na uzalendo kuliko mwenye gazeti na waandishi wake.

Kama uzalendo wao ni kule kushiriki au kunyamazia ufisadi, wizi wa mali ya umma, utekaji na utesaji wa raia, na uzalendo, basi watakuwa wako sahihi.

Lakini ukweli uko palepale. Vitendo hivi vya kufungia magazeti havitaishia kwa kufungia MwanaHALISI, Mtanzania na Mwananchi pekee; watafungia Tanzania Daima, MAWIO, Uhuru, Nipashe na vyombo vingine vya habari.

Gazeti linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), litafungiwa kwa kuwa “wenye muwasho” wa kufungia vyombo vya habari, wako mbioni kufungia Tanzania Daima.

Kwa kuwa Tanzania Daima linamilikiwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa Chadema, wenye muwasho wa kufungia magazeti, watalazimika kufungia Uhuru ili kuhalalisha kifungo cha Tanzania Daima.

Kwa kuwa mlengwa mkuu ni Tanzania Daima, basi hapo utasikia gazeti hilo likifungiwa miaka miwili, huku Uhuru likifungiwa wiki mbili. Wanajua kufungia Tanzania Daima pekee, kutaibua kelele nyingi kutoka kwa wananchi na makundi mengine.

Ni kama walivyofungia vituo vya radio – Radio Imani ya Morogoro na Radio Neema ya Mwanza  kwa muda wa miezi sita.

Taarifa zinasema, serikali ililazimika kufungia Radio Neema kwa kuwa kufungia Radio Imani pekee, kungeibua sokomoko kubwa la waislamu.

Wenye muwasho wa kufungia vyombo vya habari, wakimaliza kazi hiyo, watafunga makanisa na misikiti. Nayo misikiti na makanisa ikiisha, watafunga midomo masheikh, mapadri, wachungaji na maaskofu. Huko ndiko serikali ya kidikteta huwa inaishia.  Tusiruhusu hilo kutokea.

Wanaofungia magazeti kwa madai ya kuchapisha au kutangaza kinachoitwa na serikali kuwa ni “uchochezi,” basi wangekuwa wamefungia  kwanza televisheni ya taifa (TBC1).

Mwaka 2012 TBC walitoa takwimu kuhusu idadi ya waislamu na wakristo nchini. Taarifa hiyo ilisabisha viongozi wa taasisi za kiislamu kulalamika na wengine kuhamasisha waumini wao kususia sensa ya watu na makazi.

Pamoja na malalamiko yote hayo, TBC haikufungiwa, haikuhojiwa wala haikupewa onyo.

Msajili wa magazeti hana mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kufungia magazeti; kuyaandikia barua ya kuyaonya au kutaka kujieleza kwake. Mwenye mamlaka hayo ni waziri.

Lakini waziri wa habari ambaye siyo mwandishi wa habari, hawezi kuachwa kuwa ndiye polisi; ndiye mwendesha mashtaka wa serikali (DPP) na ndiye jaji.

Hastahili kuwa ndiye anayejua chombo fulani kimekiuka maadili. Ndiye anayesikiliza kesi na ndiye anayeamuru gazeti kufutwa, kufungiwa au kusimamishwa kwa muda anaopenda. Hiyo si haki.

Ni vema basi, kesi Na. 34 iliyofunguliwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited mwaka 2009, kupinga sheria ya magazeti, ikasikilizwa kwa haraka na mahakama.

Hii itasaidia kupatikana tafsiri sahihi ya mamlaka ya kufungia magazeti, kusajili, kuonya, kuzuia gazeti kuchapishwa kwenye mtandao na mbwembwe nyingine za msajili.

Hukumu ya kesi hii itasaidia kuzuia wenye malengo binafsi, kutumia madaraka yao kupora haki ya uhuru wa kupata, kukusanya na kusambaza habari.

error: Content is protected !!