December 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gazeti la Tanzania Daima latua kwa Waziri Bashungwa

Spread the love

 

UONGOZI wa Gazeti la Tanzania Daima, umefanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumanne, tarehe 13 Aprili 2021, ofisini kwa Waziri Bashungwa, jijini Dodoma ambapo Tanzania Daima, limewakilishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Gervan Lyenda.

Tanzania Daima ni miongoni mwa magazeti ambayo yalikutana na rungu la serikali kwa kulifutia leseni ya uchapishaji tarehe 24 Juni 2020 na sasa Waziri Bashungwa, amekutana nalo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, la kuangalia sekta ya hanari ikiwemo vyombo vya habari.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari alifuta leseni ya gazeti hilo ikiwa ni baada ya kulionya gazeti mara kadhaa huku gazeti lenyewe lililazimika kuomba radhi.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya habari imesema, Lyenda amemweleza Waziri Bashungwa kuwa “gazeti limeajiri watu 90 na wanahangaika kwakukosa leseni, tumejifunza na hatutorudia makosa.”

“Asante kwa kutusikiliza hii ni fursa kubwa kwetu, maana miezi zaidi ya nane ni mingi sana na hatujafanya kazi yoyote.”

Waziri Bashungwa amewapa wito wakuheshimu tasnia ya habari kwakuwa wote tunajenga nchi moja akisema “watanzania wa sasa wameamka, wanajua lipi ni baya na lipi ni zuri sasa kama unatoa habari zakupotosha tu utakuwa unawakosea haki yao ya kuhabarishwa”.

Pia, Waziri Bashungwa ametoa wito kwa wadau wa tasnia ya habari kuunga mkono dhamira ya Rais Samia kuona haki ya uhuru wa habari inaendana na wajibu na uzingatiaji sheria, kanuni na misingi ya taaluma ya habari.

Magazeti mengine ambayo yako kifungoni ni Mseto, Mawio na MwanaHALISI ambapo mkurugenzi wake, Saed Kubenea amekwisha kwenda Dodoma kuonana na Bashungwa.

error: Content is protected !!