WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, amekutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea kuzungumzia tasnia hiyo ya habari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kubenea, aliyewahi kuwa mbunge wa Ubungo 2015-2020, alifika ofisini kwa Bashungwa, jana Ijumaa tarehe 9 Aprili 2021, jijini Dodoma, akiitikia wito wa waziri huyo, alioutoa hivi karibuni.
Ni baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuagiza kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa huku akisisitiza lazima, vizingatie sheria na kanuni za uendeshaji wa tasnia hiyo nchini.
Waziri Bashungwa, aliagiza wamiliki wa magazeti ambayo yalifungiwa kufika ofisini kwake ili kujadiliana na kuona jinsi ya kumaliza changamoto zilizokuwapo.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo baada ya majadiliano kati ya waziri na Kubenea ambaye kampuni yake inachapisha Gazeti la MwanaHALISI na Mseto yaliyofungiwa, imesema Bashungwa ametoa wito kwa wadau wa tasnia ya habari kuunga mkono dhamira ya Rais Samia kuona haki ya uhuru wa habari inaendana na wajibu na uzingatiaji sheria, kanuni na misingi ya taaluma ya habari.
Gazeti la MwanaHALISI lilifungiwa na Serikali, Septemba 2017 kwa miaka miwili. Lilifungua kesi ndani na katika Mahakama ya Kuu ya Tanzania na kushinda kesi, wakati gazeti Mseto lilifungua kesi Mahakama ya Afrika Mashariki na kushinda pia, ila hayakufanikiwa kurejea mtaani mpaka sasa kutokana na kutopata leseni ya uchapishaji.
Leave a comment