January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gazeti la MAWIO laliliwa

Spread the love

GAZETI la MAWIO bado linapiganiwa, Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) anaeleza kwamba, kuna kila sababu ya kulifungulia ili liendelee na kazi yake nzuri kwa taifa, anaandika Happyness Lidwino.

Anasema, hatua ya serikali kulifungia gazeti hilo imekiuka kipengele cha 19 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) pia kipengele cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinatoa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Olengurumwa ametoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es kuhusu hali ya wanahabari na uhuru wa habari Tanzania.

Serikali kupitia Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ililifungia gazeti la MAWIO tarehe 15 Januari mwaka huu kwa madai ya kuandika habari za uchochezi.

Olengurumwa ameiomba serikali kuangalia upya uamuzi huo na kwamba adhabu iliyotoa haiendani sambamba na kile kinachoelezwa kuwa kosa.

Mratibu huyo amesema kuwa, serikali inaweza kulifungulia gazeti hili na hata kulipa adhabu nyingine ndogo sambamba na kuhakikisha Sheria ya Vyombo vya Habari na Sheria ya Haki ya kupata taarifa, inatengenezwa kwa muundo ambao unazingatia mapendekezo ya wadau ili nchi iweze kuwa sheria inayozingatia viwango vya Kimataifa.

Ametumia nafasi hiyo kuviomba vyombo vya habari kushirikiana na mtandao huo ili kutafuta mbinu zitakazosaidia kuipinga sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo inakandamiza tasnia ya habari nchini.

Olengurumwa amesema, wao kama mtandao wamebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kupata habari kutokana na sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo inakiuka uhuru wa habari na kupata taarifa nchini.

“Kwanza tunampongeza Rais wetu John Magufuli kwa juhudi za kupambana na rushwa na kupambana na matumizi holela ya mali za dhuluma, lakini katika siku hizo 100 za utendaji wake, kama mtandao tumebaini mapungufu mbalimbali ambayo yanakiuka haki za binadamu,” amesema Olengurumwa na kuongeza;

“Tunaona mambo kadhaa kama suala la uhuru wa habari kuendelea kukandamizwa, mambo ya demokrasia na utawala bora likiwemo suala la Zanzibar kuchukua muda mrefu katika kukamilisha mchakato wake, hivyo basi kama mtandao tunaomba vyombo vya habari kuungana nasi katika kutafuta namna ya kuipinga sheria ya magazeti inayovunja na kukiuka Uhuru.”

Amesema, kwa miaka mingi Sheria ya Magazeti imekuwa ikiorodheshwa kama sheria inayokiuka uhuru wa kujitosheleza kutokana na kumpa waziri mwenye dhamana nguvu kubwa kutoa maamuzi.

“Sheria hii kwanza ilirithiwa kutoka katika uongozi wa Mkoloni na ilitengenezwa kwa kusudio la kukandamiza sauti ya watawaliwa, tunaiomba serikali kuchukua hatua za haraka za kurekebisha vifungu vinavyopinga uhuru ama la sheria iangaliwe upya,” amesema.

Akitolea mfano wa gazeti la Mwanahalisi, Mwananchi na Mtanzania ambayo yalisitishwa kwa muda, na sasa gazeti la MAWIO lililofutwa kutokana na taarifa waliyoichapisha ikilalamikiwa kuwa ni ya kichochezi, Mratibu huyo amesema, suala hilo limeonesha kuwa sheria hiyo imeendelea kutumika vibaya.

Amesema, kwa kuzingatia sheria na vigezo vya kimataifa, ufutwaji wa gazeti la MAWIO umekiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na katiba ya nchi.

error: Content is protected !!