December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gavana Sonko ang’olewa rasmi madarakani

Spread the love
BUNGE la Seneti nchini Kenya, limepiga kura kumuondoa malakani aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Mubuvi Sonko, kufutia kupatikana na matumizi mabaya ya ofisi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Wajumbe 27 walipiga kura ya kuunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani Sonko, baada ya kuidhinisha mashtaka yote manne yaliyowasilishwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Bunge la Kaunti ya Nairobi, lilipiga kura ya kumfukuza kazi Bw. Sonko, tarehe 3 Desemba mwaka huu.

Sonko alituhumiwa kwa ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya madaraka, utovu wa nidhamu na uhalifu chini ya sheria.

Hatua ya Bunge hilo kumvua madaraka Sonko, imekomesha miaka mitatu ya utawala wake uligubikwa na utata.

Kuondolewa madarakani kwa Sonko kumetoa nafasi kwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Ben Mutura kushikilia wadhifa huo hadi uchaguzi wa gavana mpya na naibu wake utakapofanyika katika kipindi cha siku 60 zijazo.

Mike Mubuvi Sonko, alizaliwa Februari 1975. Alikuwa mbunge wa Makadara kati ya mwaka 2010 hadi 2013 na kuchaguliwa Seneta wa Nairobi, Machi 2013.

Alichaguliwa kuwa gavana wa Nairobi Agosti 2017.

Rais Uhuru Kenyatta

Ganava aliyeondolewa madarakani – Mike  Sonko – siyo mgeni katika masuala yenye utata. Hivi karibuni, maafisa wa magereza nchini Kenya, walimshtaki kwa kutoroka kutoka jela miaka 20 iliyopita.

Sonko amewahi kukiri hadharani kutoroka gerezani wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na baadhi ya vyombo vya habari.

Sonko alichaguliwa kuwa gavana wa Kaunti ya Nairobi mwaka 2017, kupitia chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, wawili hao wametofautiana kufikia hatua ya Rais Kenyatta kushinikiza mageuzi yaliyochangia kupunguza majukumu makuu ya Kaunti ya Nairobi kuhamishiwa serikali ya kitaifa.

Rais Kenyatta alimteua jenerali wa kijeshi kuendesha shughuli za kaunti, hali iliyomfanya Sonko kuwa gavana “asiye na mamlaka.”

Sonko, ambaye alishiriki hafla ya kukabidhi baadhi ya majukumu ya kaunti kwa serikali kuu, baadaye alidai kwamba wakati wa kusaini nyaraka za kukabidhi majukumu hayo, alikuwa mlevi.

Sonko alijipatia umaarufu kutokana na mtindo wake usio wa kawaida alipokuwa mbunge wa Makadara, Nairobi. Anafahamika kwa kuvalia vito, mikufu na bangili za thamani.

Alipokuwa mbunge, alikuwa akiandamana ‘kutetea wanyonge’ na wachuuzi walipokuwa wanafurushwa kutoka maeneo yao ya kazi na serikali ya jiji.

Alipokuwa Seneta, alianzisha kundi kwa jina “Sonko Rescue Team” ambalo lilikuwa likitoa huduma kama vile maji, matibabu na misaada wakati wa mazishi.

Wakati mmoja alipoitwa kusaidia familia zilizokuwa zimeathiriwa na bomoa bomoa jijini mwaka 2014, alimpigia simu Rais Kenyatta na kumuweka kwenye kipaza sauti. Rais alitoa agizo ubomoaji usitishwe.

Alipoingia uongozini kama gavana wa Nairobi, ameonekana kuchukua hatua ambazo zinaenda kinyume na aliyokuwa akitetea.

error: Content is protected !!