Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Gari litakaloziisha mzigo faini Mil 34, jela miaka mitatu
Habari Mchanganyiko

Gari litakaloziisha mzigo faini Mil 34, jela miaka mitatu

Spread the love

SHERIA ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajia kuanza kutumika nchini Januari 2019 huku ukomo wa adhabu kwa makosa ya usafirishaji utakuwa ni dola za Marekani 15,000 (zaidi ya Sh. 34 milioni). Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Joseph Nyamhanga wakati wa kufungua kikao kazi cha wadau wa sekta ya ujenzi utakaojadili kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.

Amesema sheria hiyo ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017 katika usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya barabara nchini zitaanza kutumika mwakani ikiwa ni kutekeleza matakwa ya Jumuia ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania na Burundi bado hawajaanza kuitumia.

“Katika kipindi hiki cha mpito, kazi zitakazofanyika nikutoa elimu kwa jamii ambapo elimu hii itatolewa katika kanda zote na pia kubadili mifumo kwenye mizani ili kwenda sambamba na sheria hiyo.”

Aliongeza: “Kwa kiasi kikubwa sheria hii inafanana na Sheria tunayotumia sasa nchini Tanzania, tofauti katika baadhi ya maeneo,” amesema.

Nyamhanga amesema kwa sheria hiyo mpya ukomo wa mtaimbo wenye matairi mapana utakuwa tani 8.5 badala ya tani 10 za sasa.

“Pia kutakuwa na mfumo wa kuweka kumbukumbu za makosa ya msafirishaji na anayezidisha uzito ambao hatimaye unaweza kusababisha gari kufungiwa kufanya usafirishaji kwa muda au moja kwa moja.”

Nyamhanga amesema kwa sheria hiyo mpya pia kutakuwa na adhabu kwa makosa ya usafirishaji hadi ukomo wa dola za Marekani 15,000 au kifungo kisichozidi miaka 3 au vyote kwa pamoja.

“Aidha, adhabu hizo zitahusu pia watumishi wa mizani wanakula njama na wasafirishaji ili kukwepa kulipa tozo ya kuzidisha uzito. Sheria ya sasa suala la kifungo au vyote kwa pamoja, lakini sasa limeongezwa,” alisema.

Nyamhanga amesema sheria hiyo pia inahusu gharama za utunzaji gari iliyokuwa na makosa katika maeneo ya mizani baada ya siku tatu kulipa ni dola za Marekani 50 kwa siku badala ya dola za Marekani 20 kwa siku kwenye sheria ya sasa.“

Aidha, gharama ya kuendelea kuegesha gari ndani ya yadi ya mizani baada ya kulipa tozo ya uzalishaji uzito ni dola za Marekani 50 kwa siku,” alisema.

Nyamhanga amesema sheria mpya pia inataka wasafirishaji kuhitaji vibali mahususi vya kusafirisha mizigo isiyo ya kawaida katika makundi mbalimbali.

Akifafanua aina ya vibali, Nyamhanga amesema ni kwa mizigo iliyozidi vipimo kwa mujibu wa Sheria na ile ambao unaweza kugawanyika lakini unahitaji umakini zaidi na vifaa maalum katika ushushaji wake.

Pia vibali vitatakiwa kuombwa kwa mzigo ambao haugawanyika na umezidi kiwango cha uzito unaoruhusiwa kisheria na ile ambayo ni hatarishi kwa afya na usalama katika usafirishaji wake kwa njia ya barabara.

“Pia vitaruhusu mzigo ambao unaweza kuhama kutoka sehemu moja ya gari hadi sehemu nyingine wakati gari likiwa kwenye mwendo au limesimama.

Aliongeza: “ Vibali vya kusafirisha mizigo vitalipwa dola za Marekani 10 badala ya dola za Marekani 20 kwenye Sheria inayotumika sasa. Gharama ya vibali imeshuka, lakini kuna masharti makubwa zaidi ili kuzilinda barabara zetu.”

Nyamhanga alisema Sheria ya mpya na kanuni zake ina mashariti magumu na adhabu kali kwa makosa ya uzidishaji uzito wa magari na makosa mengine ya usafirishaji.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wasafirishaji kutii na kuzingatia kikamilifu matakwa ya sheria kwa kutozidisha uzito wa magari ili kuepuka adhabu kali, lakini pia kuzifanya barabara zidumu kwa muda mrefu zaidi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

THRDC yaongeza mkataba wa ushirikiano na ABA

Spread the love  MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),...

error: Content is protected !!