July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Galawa awashauri wakutubi

Spread the love

WATUNZA kumbukumbu, nyaraka na Takwimu nchini (WAKUTUBI), wametakiwa kutoa taarifa sahihi kwa jamii hususani za kiuchumi badala ya kuzificha makabatini, anaandika Dany Tibason.

Kauli hiyo ilitolewa na Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alipokuwa akifungua warsha na mkutano mkuu wa umoja wa wakutubi Tanzania uliofanyika Dodoma.

Galawa amewaambia watunza kumbukumbu kwamba wanatakiwa kuhakikisha wanatoa taarifa muhimu kwa jamii hususani taarifa za kilimo, ufugaji na hali ya hewa ya kilimo.

Katika mkutano huo Galawa amewaasa wakutubi wengi wamekuwa na tabia ya kuweka taarifa muhimu makabatini badala ya kutoa taarifa hizo kwa jamii ili ziweze kuwasaidia.

“Kuna tatizo kubwa kwa watanzania kutokuwa na tabia ya kutopenda kusoma, lakini tatizo hilo linawakumba hata wakutubi kwani zipo taarifa nyingi za muhimu ambazo zinatakiwa kutolewa kwa jamii lakini hata wakutubi wenyewe hawazijui.

“Unaweza kushangaa pale ambapo unaweza kuuliza taarifa fulani ndani ya maktaba lakini cha ajabu mkutubi akakuambia hata yeye hajui, nataka kuwaambia na nyie jengeni tabia ya kujisomea ili muweze kuishawishi jamii ili iweze kutumia maktaba kwa faida zaidi,” amesema Galawa.

Mbali na hilo aliwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa malengo ya kufikiri mbali zaidi na kuwa na mawazo ya kukuza pato la mtanzania.

“Kwa sasa serikali ya awamu ya tano inakusudia kukuza uchumi ili kuwepo kwa uchumi wa kati kwa maana hiyo ni vyema wakutubi kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo ili taarifa zao ziwe na malengo ya kuchochea uchumi katika sekta zote,” amesema Galawa.

Kwa upande wake Richard Mhaha, Mwenyekiti wa Chama Wakutubi Tanzania, amesema kwa sasa taarifa ambazo zinatolewa zinalenga kukuza na kutangaza rasilimali zilizopo nchini.

Amesema Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zikitolewa taarifa sahihi na zenye ushawishi zinaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa ajili ya kukuza uchumi.

Alitolea mfano wa rasilimali zilizopo nchini ambazo ni rasilimali asili iwapo zitatangazwa vizuri na kuonesha umuhimu wake ni wazi kwamba wanaweza kuwahamasisha wakulima, wafugaji pamoja na jamii nyingineo kuchangamkia fursa husika badala ya vijana kukaa kijiweni.

error: Content is protected !!