August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gaidi auawa ubalozi wa Marekani Kenya

Spread the love

POLISI nchini Kenya, wamempiga risasi mshukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab aliyejaribu kuingia kwa mabavu ndani ya ubalozi wa Marekani, eneo la Gigiri jijini Nairobi, anaandika Wolfram Mwalongo.

Mshukiwa huyo alifika katika geti la ubalozi huo akitaka kuingia ndani licha ya kuzuiwa na polisi, baadaye alimshika kichwani askari mmoja aliyekuwa getini hapo, kitendo kilichosababisha askari waliokuwepo kumpiga risasi.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi huo umekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba tukio hilo ingawa imedokeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa na mamlaka husika za Kenya.

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini Kenya wamechukua vipimo vya mshukiwa huyo kwa uchunguzi zaidi, ingawa taarifa za awali zimeeleza kuwa mtu huyo alikuwa na kadi (laini ya simu) kwenye pochi yake ingawa hakuwa na simu.

Ulinzi katika balozi za Marekani katika nchi mbalimbali za Afrika umeimarishwa zaidi hasa tangu kutokea kwa mashambulizi ya ofisi za ubalozi za taifa hilo katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya na Tanzania mnamo mwaka 1998 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

Tarehe 7 mwezi Agosti mwaka 1998 saa 3:30 asubuhi, ofisi za ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya zilishambuliwa na watu 213 kuuawa huku wengine zaidi ya 3,000 wakijeruhiwa.

Wakati huo huo saa 3:40 asubuhi ya siku hiyo Jijini Dar es salaam, ofisi za ubalozi wa taifa hilo pia ulishambuliwa na kusababisha watu 11 kuuawa na wengine zaidi ya 85 kujeruhiwa. Matukio hayo yalitekelezwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda chini ya aliyekuwa kiongozi wake Osama bin Laden.

error: Content is protected !!