DAKTARI Hamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii amesitisha mpango wake wa kupeleka fuvu la mtu wa kale katika Makumbusho ya Olduvai, Ngorongoro kutokana na sababu za kisalama. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Dk. Kigwangalla ametoa kauli hiyo leo tarehe 14 Juni 2019, katika akaunti yake ya Twitter, ikiwa ni siku moja tangu Rais John Magufuli kueleza kwamba, fuvu hilo lilikuwa kwenye mpango wa kuibiwa.
Rais Magufuli wakati akizungumza na wavumbuzi wa mitambo ya umeme Ikulu, Jijini Dar es Salaam jana tarehe 13 Juni 2019 alisema “nimesikia hata fuvu la mtu wa kale lilikuwa kwenye ‘plan’ (mpango) ya kuibiwa, hii ndiyo Tanzania.”
Wakati nikipokea tuzo ya Hifadhi Bora Afrika iliyotolewa na World Travel Awards kwa Serengeti, nilitangaza kuwa Mwaka huu tutasherehekea miaka 60 ya #Zinjanthropus, na niliahidi kulipeleka fuvu halisi makumbusho ya Olduvai, Ngorongoro. Kwa sababu za kiusalama hatutolipeleka! pic.twitter.com/psRF6GecgC
— Dr. Hamisi Kigwangalla (@HKigwangalla) June 14, 2019
Katika andiko lake kwenye akaunti ya Twitter, Dk. Kigwangalla amesema, alipanga kulipeleka fuvu hilo kwenye maadhimisho ya miaka 60 tangu kuvumbuliwa kwa fuvu la binadamu wa kale duniani la Zinjanthropus, yaliyopangwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Wakati nikipokea tuzo ya Hifadhi Bora Afrika iliyotolewa na World Travel Awards kwa Serengeti, nilitangaza kuwa mwaka huu tutasherehekea miaka 60 ya Zinjanthropus, na niliahidi kulipeleka fuvu halisi makumbusho ya Olduvai, Ngorongoro. Kwasababu za kiusalama hatutolipeleka! ,” ameandika Dk. Kigwangalla.
Mapema mwezi huu Dk. Kigwangalla aliwaahidi Watanzania kwamba, fuvu hilo litawekwa hadharani kwa muda wa siku tano kuanzia Julai 17 mwaka huu, na kuwataka Watanzania kutumia fursa hiyo ili kuliona fuvu hilo linalohifadhiwa katika sehemu maalum na serikali.
Leave a comment