Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Freeman Mbowe, Zitto Kabwe kuiteka Kisutu wiki nzima
Habari za SiasaTangulizi

Freeman Mbowe, Zitto Kabwe kuiteka Kisutu wiki nzima

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu itaendelea na usikilizaji wa kesi  za uchochezi zinazowakabili viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo, wiki nzima mfululizo. Anaandika Faki Sosi …(endelea)

Mahakama hiyo itaendelea na usikilizaji wa kesi hizo kuanzia Jumatatu ya tarehe 13 hadi Ijumaa tarehe 17 Mei 2019.

Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba imepanga kusikiliza mfululizo kesi namba 112 ya mwaka 2018 inayowakabili viongozi wa Chadema kuanzia tarehe 13, 14, na 15 Mei 2019. Kesi hiyo ipo kwenye hatua ya ushahidi baada ya tarehe 17 Aprili 2019, upande wa Serikali kutoa ushahidi wake.

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Zanzibar, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Bara.

Wengine ni Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Siku hiyo, shahidi wa kwanza alikuwa ni Mrakibu wa Jeshi la Polisi (SSP), Gelard Ngichi aliyetoa ushahidi kwenye mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi.

SSP Ngichi ambaye ni Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, aliieleza mahakama kwamba yeye alikuwa na jukumu la kusimamia mikutano yote ya kisiasa ndani ya Mkoa huo.

Na kudai kuwa tarehe  16 Februari 2017, alisimamia ufungaji wa kampeni za vyama vya siasa kutokana na uchaguzi wa mdogo wa jimbo la Kinondoni uliofanyika tarehe 17, Februari mwaka 2017.

Alidai kuwa kwenye kampeni hizo viongozi wa Chadema waliandamana bila kibali na kusababisha vurugu zilizosababisha askari wake watumie risasi za moto, walizua taharuki na waliongea maneno ya uchochezi.

Lakini shahidi huyo aliulizwa maswali na upande wa utetezi uliowakilishwa na Wakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, Jeremia Mtobesya, John Mallya na Hekima Mwasibu.

Shahidi aliulizwa kama kuna mtu yoyote aliyeathirika na maandamano hayo akajibu wapo askari wawili  na alisikia taarifa ya kuuawa kwa raia mmoja alimtaja kuwa ni Akwelina Akwelini.

SSP Ngichi aliulizwa kama kuna mtuhumiwa yoyote aliyefikishwa mahakamani juu ya mauaji ya Akwelina alijibu hajui.

Licha ya Mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupanga kusikiliza mfululizo kesi hiyo, pia itasikiliza kesi namba 327 ya mwaka 2018 inayomkabili Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo tarehe 16 na 17 Mei 2019, ambapo upande wa Serikali utaendelea kupeleka mashahidi mahakamani hapo.

Awali tarehe na 23 na 25 Aprili 2019, upande wa mashtaka ulimfikisha shahidi wa kwanza, SSP John Malulu,  Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, akiongozwa na Nassoro Katuga Wakili wa Serikali Mkuu, na Tumaini Kweka. Kwa ajili ya kutoa ushahidi Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.

Katika ushahidi wake, SSP Malulu aliieleza Mahakama kwamba yeye akiwa kama Mkuu wa Upelelezi, aliandika maelezo ya awali ya ufunguzi wa kesi juu ya maneno aliyodai kuwa ni ya uchochezi ambayo yalikuwa na lengo la kulichonganisha Jeshi la Polisi na Wananchi.

SSP Malulu amedai kuwa tarehe 28 Oktoba, 2018, alimuona Zitto Kabwe akijitanabaisha kama kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo akiongea kwenye mkutano wa vyombo vya habari na kutoa maneno ya uchochezi.

Alidai kuwa maneno hayo hakuyatilia maanani mpaka kesho yake tarehe 29 Oktoba, 2018 alipoona kundi la watu maeno ya Manzese Tip Top  na Kimara Korogwe wakijadili kwa hasira na jazba maneno ya Zitto, ya kuwa Jeshi la Polisi limekuwa la kinyama na wauaji.

SSP Malulu alidai kuwa, makundi hayo mawili yamemfanya atilie maanani mkutano wa Zitto na aliporejea ofisini kwake Osterbay aliita maofisa wa upelelezi na wanaohusika na makosa ya mtandaoni na kuanza kufuatilia na baadaye kumkamata Zitto kisha kumpeleka mahakamani.

Upande wa utetezi uliongozwa na wakili Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya na Steven Mwakibolwa.

Wakili Kibatala alimuuliza shahidi juu ya elimu yake, akadai kuwa yeye ni darasa la saba, na baadae alimuuliza juu ya ukweli kuhusu mauaji ya Uvinza na Nguruka, alikiri kutokea kwa askari wawili.

Pia, Wakili Kibatala alimuuliza kuhusu mauaji hayo kuzungumziwa na Bunge na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwenda maeneo hayo pamoja na baadhi ya maofisa kuhamishwa kwa sababu ya matukio hayo, akajibu kuwa hafahamu.

Vile vile, Wakili Mtobesya alimuliza shahidi juu mawasiliano ya shahidi na Mkuu wa Upelelezi wa Kigoma ambaye amemtaja kwenye ushahidi na kama anarekodi ya mawasiliano yao. Shahidi huyi alijibu kuwa hana rekodi yoyote mwisho.

Wakili Mwakibolwa alimuuliza shahidi kuwa alipotoka kwenye hayo makundi mawili, ambalo moja alieleza kuwa lina watu takribani 15 alienda wapi, akajibu kwenye kituo cha Polisi cha Gogoni Kimara ndipo alimuuliza alikwenda kufanya shughuli gani shahidi alijibu alikwenda kwa shughuli zake.

Mwakibolwa alimuuliza shahidi kuwa yale aliyoyaona kule sio kitu kikubwa ndio maana akaenda Kimara na ishu zake, Shahidi alijibu hapana na kwamba alienda kuhakikisha ulinzi.

Kutokana na kesi hizo mbili Mahakama ya Kisutu itakuwa katika mchakamchaka wa wiki nzima kufuatia kesi hizo kuwa na mvuto kwa jamii.

MwanaHALISI ONLINE itakuwepo mahakamani hapo kuhakikisha kuwa haupitwi na taarifa yoyote juu ya mwendelezo wa kesi hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!