November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fomu serikali za mitaa: mbwembwe marufuku

Suleiman Jafo, Waziri wa Tamisemi

Spread the love

MBWEMBWE na shamrashamra zilizozoeleka katika uchukuaji fomu za kugombea ngazi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini, zimepigwa marufuku. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Vyama vya siasa vilivyoweka dhamira ya kugombea kwenye uchaguzi huo, wagombea wake watalazimika kwenda kimya kimya kuchukua fomu na kurejea walikotoka.

Msimamo huo umetolewa na Suleiman Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMAI), leo tarehe 28 Oktoba 2019 mbele ya wanahabari jijini Dodoma.

“Hairuhusiwi kwenda kwa mbwembwe wala shamrashamra katika uchukuaji fomu,” amesema Jafo na kuongeza “kwenda kwa mbwembwe kutapelekea kuanza kufanya kampeni kabla ya muda wake.”

Waziri huyo amesema, kwa mujibu wa taratibu, fomu za kugombea zitaanza kutolewa kesho tarehe 29 Oktoba 2019, kwenye uchaguzi huo, nafasi zitazogombewa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo.

Nafasi zingine ni mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa Kamati ya Mtaa (wanawake na wanaume), wajumbe wa kamati ya mtaa (wanawake) katika Mamlaka za Miji, Mwenyekiti wa Kijiji, wajumbe wa Halmshauri ya Kijiji (wanawake na wanaume), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (wanawake) na wenyeviti wa witongoji katika mamlaka za wilaya.

Jafo amesema, wagombea wanaruhusiwa kusindikizwa wakati wa kuchukua fomu na si kufanya jambo lingine, na kwamba ukomo wa kuchukua fomu hizo ni tarehe 4 Novemba 2019. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Novemba 2019.

Hata hivyo ameshauri vyama vya upinzani kuwasaidiwa wagombea wao kujaza fomu, kwa kuwa kumekuwepo na malalamiko pale wanapoenguliwa kutokana na kushindwa kujaza fomu hizo kwa namna inavyopaswa.

“Viongozi wanashindwa kuwasaidia wagombea wao katika kujaza fomu, mwisho wa siku hujikuta wamekosea. Sasa kwa kuwa muda upo wa kutosha, wakajipange vizuri.”

error: Content is protected !!