January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fitina za kisiasa

Hassan Nassor Moyo

Hassan Nassor Moyo

Spread the love

[note color=”#F6F6F6″]ALHAMISI iliyopita, tulichapisha sehemu ya kwanza ya mjadala wa kongamano lililoitishwa na Kamati ya Maridhiano Zanzibar lililofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Bwawani. Ni katika kongamano hilo, Mansour Yusuf Hamid, mwakilishi wa Kiembesamaki, Unguja alipopewa nafasi ya kuzungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuvuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hapa alikuwepo Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassor Moyo. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya hotuba yake juu ya “fitina za kisiasa.” Endelea.[/note]

KILA uchaguzi Visiwani, watu wetu wanakuwa roho zao zipo juu. Wengine wanadiriki kuhama nchi…kupisha uchaguzi kwa sababu wanajua uchaguzi wa Zanzibar hauwezi kwenda salama.

Ndiyo maana Mzee Karume (Abeid Aman Karume, rais wa kwanza wa Zanzibar) akatangaza wakati mmoja, Unguja haujii uchaguzi mpaka baada miaka 50… fitna hiyo! Watu watakuwa wanauana, wanapigana.

(Hata baadaye…fitina iliendelea) Tulikuwa hatuzikani hapa. Mimi CCM (Chama Cha Mapinduzi) siendi kwa huyu CUF (Chama cha Wananchi). Tulifikia hatua ya kutia vinyesi ndani ya kisima na mengine mnayajua. Fitna ya vyama vingi hiyo.

Kwa hiyo, ninachojaribu kuwaeleza ndugu wananchi, ni kwamba hakuna kitu kibaya kama fitna. Chama chetu cha CCM, chama chetu cha CUF, vikachagua tume ya CUF na CCM kutengeneza utaratibu wa kuondosha hizi fitna na fujo Visiwani, maana Unguja ndio kwenye opposition (opozisheni -upinzani).

Nawaambia Unguja ndio kwenye opozisheni. Ukisikia kwenye opozisheni kweli ya vyama, siyo Bara (Tanganyika), ni Unguja. Hapa kulikuwa na opozisheni kweli na mpaka sasa tunaendelea nayo.

Hapa pameundiwa miafaka mitatu; tena na watu wa nje kuja na mapesa kulipa wajumbe wa zile kamati, ili ipatikane suluhu hapa Unguja, lakini utekelezaji hakuna. Wanatia mkataba; viongozi wetu wanakubaliana, lakini hakuna utekelezaji. Mnanielewa ndugu zangu?

Mkataba wa mwisho alikuja hapa Rais Mkapa  (Benjamin Mkapa) na wakati ule Rais Aman (Aman Abeid Karume) vilevile, wanaoshuhudia hapa kina Abubakar na kina Moyo hao, wanatia saini mkataba wa maelewano wa muafaka.

Ilifikia hivyo, viongozi wanashuhudia wadogo zao wanatia mkataba wa maelewano. Hakuna kilichofanyika. Kwa nini? Kwa sababu, hakukuwa na ile ithibati. Nia safi ya kutengeneza nchi yao hii Zanzibar ili itulie.

Haikuweko hiyo, kwa sababu kulikuwa na mchanganyiko wa Bara na Visiwani wako mlemle wanatengeneza lile jambo. Wengine hawataki Unguja itulie, hawataki kabisa… kwa hiyo watafanya kila hila na kila mbinu lile jambo lisifanyike; na ndivyo ilivyokuwa, ndivyo ilivyokuwa hivyo.

Maana haiwezekani watu wazima wanakaa kitako, wanazungumza, wanapanga, wanakubaliana, wanatia signature (saini) yao, kwa jambo lao, halafu utekelezaji ushindikane. Mnaona? Kulikuwa na nia safi pale? Hapana! No! Hakukuwa na nia safi. Ulikuwa mchezo wa kitoto tu; hapakuwa na nia safi kabisa.

Lakini nataka kuwambieni, baada ya Abeid Aman Karume, baada ya Seif (Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wa CUF), kusahau nafsi zao, kusahau ukubwa wao, kusahau utukufu wao na kuiangalia Zanzibar, jambo hili limewezekana.

Haikuwa kazi rahisi hiyo. Lakini Seif na Karume wakasema wao watakufa siku moja, lakini Zanzibar haifi; wakasema wao siku moja wataondoka katika madaraka ya urais au ukatibu mkuu; lakini Zanzibar itabaki palepale.

Wakasema siku moja vyama vyetu vitaondoka, vitakufa; lakini Zanzibar itabakia palepale. Na mifano ipo, ASP (Afro Shirazi Party), ipo wapi, si imekufa? Na tukasema wenyewe kwamba hatukuvunja TANU (Tanganyika African Unioun) au ASP kwa kuwa ilifanya makosa, hapana.

Tulivunja vyama hivyo kutafuta umadhubuti zaidi, lakini leo iko wapi? Huo umadhubuti upo wapi? Kumejaa fitna tele… au nasema uongo?

Kwa hiyo, Aman na Seif wakaiangalia nchi, wakasahau ukubwa wao, vilemba vyao vile wakavisahau, wakasema kwanza nchi; ndiyo maana wakachagua kamati hii mnayoiona hapa, na leo tumeamua tusiweke mtu yoyote ambaye siyo mwanachama wetu…mtupige picha hapa za tv (televisheni) na kila kitu, muende huko nje mtupe majina mnayotaka.

Kwa hiyo wakaamua, Rais Aman na katibu mkuu, Maalim Seif wasahau ukubwa wao, wasahau mambo yao, waiangalie Zanzibar kwanza, wakachagua timu hii mnayoiona hapa ya Wanaume. Tukapewa kazi moja tu ya kutafuta namna gani tunaweza kuleta maridhiano katika nchi hii na kuondosha fitna. Wakasema, “…tumechoka na fitna.”

Kuna mahala nimeambiwa mimi wakati ule siyo leo… jamaa zetu ndani ya CCM wamemuhoji Karume. Wamemwambia wewe unaunda kamati hii sisi hatujui, unataka kuuza chama? Unataka kuuza nchi?

Yeye akasema, mimi siundi kamati hii kwa maana ya kuuza nchi; mimi naunda kamati hii kwa kuwa nataka kutengeneza nchi.

Wengine walimuhoji, naye akawahoji vilevile, wakati huo zile sharubu zinamcheza. Kwamba ninyi mnaokataa hili jambo mimi nisilifanye, mnaweza kunipa ushindi wenu  wa asilimia 60? Ninyi mnaosema hapa tusiungane, mnaweza kunipa  asilimia 60 ya ushindi wangu?

Akasema miye sina haja ya kushirikiana na CUF wale. Aliwaambia hivyo mbele ya mkutano. Wale waliokuwa viranja tena kutoka Unguja walitaka kumkaba. Akawaambia mnaweza kunipa  asilimi 60 ya ushindi wangu; na nyie ushindi wetu Unguja mnaujua? Nani asiyeujua katika nyie? Wote wakanyamaza kimya.

Mimi nina habari kuwa kiongozi mmoja alisimama katika vikao vyao, mimi siyo mwanachama wa vikao vyao, mimi mwanachama wa CCM basi,  akawaambia habari niliokuwa nazo mimi, uchaguzi wa safari hii, CUF mjini (mkoa wa Mjini Magharibi) watachukua viti sita.

Aliwaambia hivyo. Wamepata viti vingapi? Siyo vinne Mjini? Amekosea? From two to four (kutoka viwili hadi vinne), lakini aliwaambia watapata sita. Sisi kazi yetu ni kelele kelele tu.

Lakini Aman akasema, no! (hapana) mimi lazima nitaunda kamati ya kufanya kazi kuondosha fitna; na akawaambia mimi hamkunichagua kule Zanzibar niwe msimamizi wa mauaji ya watu au fitna za watu. No! (hapana). Mimi kazi mlionichagulia kule ni rais wa kusimamia amani na maendeleo ya Wazanzibari.

Hiyo ndiyo kazi niliyochaguliwa kuifanya, hivyo matokeo yake ndiyo kamati hii. Tukafanya kazi kwa lillahi (udhati) usiku na mchana, senti moja hakuna. Nimekwambieni, nani amepewa senti moja?

Hatukupewa, hatukupewa, tumekuwa tunakula chakula kwa Idd (Eddy Liyami, mmoja wa wajumbe wa kamati ya maridhiano); pesa zake mwenyewe akitoa mkononi.

Lakini wao wamepewa mapesa, mengine madola, mapaundi yametoka Ulaya, wamefanya nini? Kwa sababu dhamira ilikuwa hakuna. Kulikuwa hakuna nia safi kuitengeneza Zanzibar, kuifikisha mahala hapa. Walikuwa wanataka tuendelee kulumbana wenyewe kwa wenyewe tu, kugombana tu, kuuana tu.

Basi, tukasema hapana! Aman akasema hapana!. Seif akasema hapana! Leo tumepata matunda haya. Tumeunda serikali ya pamoja, serikali ya umoja wa kitaifa. Mnataka nini tena…?

Itaendelea wiki ijayo...
error: Content is protected !!