January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Filikunjombe, wenzake waagwa Dar

Spread the love

HALI ya simanzi imetawala leo kwenye Hospitali ya Jeshi, Lugalo jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga miili ya watu watatu waliofariki dunia kwenye ajali ya Helkopta iliyotokea juzi jioni kwenye Poli la Selous akiwemo Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe. Anaandika Sarafina Lindwino … (endelea).

Nyuso za huzuni zilitawala baada ya miili ya marehemu hao kufikishwa kwenye viwanja vya hospitali hiyo ili kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki ambapo viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa walihudhuria.

Wengine waliofariki kwenye ajali hiyo ni William Silaa (rubani) Egid Nkwera, na Plasdus Haule. Miili hiyo ilifikishwa kwenye viwanja hivyo saa 5:5 asubuhi.

Viongozi waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete; Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Maliasili, Mazingira na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Waziri Kivuli wa Afya, Suzan Lyimo pia Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe.

Kafulila akiwakilisha upinzani wakati wa kutoa salamu za mwisho ameeleza kupokea taarifa za msiba wa Filikunjombe kwa masikitiko makubwa na kwamba alikuwa akipendwa na vyama vyote kutokana na umahiri wake katika kazi.

“Mbali na siasa Filikunjombe alikuwa ni rafiki yangu, mlezi wa ndoa yangu, ni mtu ambaye alikuwa tofauti na wabunge wengine wa CCM kwani alisimamia anachokiamini bila kujali nani anamtazama. Alishirikiana na viongozi wote bila kujali yupo chama gani,” amesema Kafulila.

Makamba ambaye aliwakilisha chama tawala amesema, CCM imepata pigo kubwa kwa kumpoteza Filikunjombe kwani alikuwa tegemezi katika mambo mengi ya ujenzi wa Taifa.

“Marehemu alitukumbusha wengi maana ya kuwa kiongozi na kujitambua katika uongozi. Alipigania wanyonge na kusimamia haki za binadamu bila kujali itikadi za chama. Tufate nyayo zake ili kumuenzi ikiwa ni pamoja kuikumbuka familia yake,” amesema Makamba.

Akiwakilisha Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto amesema, “kwa hakika tumempoteza mpiganaji na hakuna njia nyingine ya kumuenzi zaidi ya kuendeleza mapambano yake. Kwa hakika alikuwa kiongozi bora, namfahamu vizuri kwa umahiri wake tangu tulipokuwa bungeni.”

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Membe amesema, “msiba huu umelitingisha Taifa kwa kuwa alikuwa kipenzi cha pande zote. Tumepoteza jembe lililotegemewa na wananchi.”

Spika Makinda akitoa salamu kwa niaba ya Bunge amesema, marehemu alikuwa ni mfano wa kuigwa kwani kazi alizofanya ndani ya miaka mitano hazimfikiwi hata na aliyekaa bungeni kwa miaka 20.

“Yeye alitumia muda mwingi kukaa na wananchi wake kuliko bungeni. Nakosa hata nguvu ya kusimama kwani mwezi huu wote umekuwa ni wa majonzi kwetu, tumepoteza wabunge wanne ndani ya mwezi mmoja. Laikini yote ni mipango ya Mungu, tuwaombee wenzetu waliotutangulia.”

Amesema, wabunge wajao waige mfano kwa marehemu na kuongeza “tuache kutungiana uongo kwa vifo vinavyotokea bali tuombeane tu kwani vifo ni mipango ya Mungu na sio binadamu.”

Aidha, Filikunjombe alifariki juzi kwa ajali ya Helikopta iliyoanguka mkoani Morogoro katika mbuga ya selous wakati akitokea Dar es Salaam kuelekea jimboni kwake.

Baada ya kuagwa, miili yote imepelekwa nyumbani kwa Filikunjombe Kijichi Wilaya ya Temeke kwa ajili ya ibada maalumu na kisha kusafirishwa kwa ndege kwenda Iringa kwa ajili ya mazishi.

error: Content is protected !!