February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Filamu ya makontena ya Makonda yaendelea

Spread the love

MAKONTENA 20 yenye samani mbalimbali yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yanayopigwa mnada na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutokana na kudaiwa kodi ya Sh. 1.2 bilioni, yameshindwa kununuliwa kutokana na wateja kushindwa kufika bei. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Wateja waliofika katika uuzwaji wa makontena hayo yaliyopigwa mnada kwa mara ya tatu leo tarehe 9 Septemba, 2018 Bandarini jijini Dar es Salaam, na Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, walilalamika kwamba thamani ya samani zilizomo kwenye kontena hizo hazilingani na bei iliyopangwa na TRA.

TRA ilipanga bei elekezi kwa kila kontena kuwa ni milioni 60 ambapo ukizidisha na idadi ya kontena 20 unapata kiasi cha bilioni 1.2 ambazo mamlaka hiyo inadai kama kodi.Lakini katika mnada huo wateja waliohudhuria walianza na bei ya milioni 5 hadi milioni 15 kwa kila kontena, hata hivyo mteja mmoja alifika bei ya milioni 40 katika kontena la 13 lililotangazwa na mwendesha mnada.

Mwendesha mnada ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Scholastica Kevela amesema wateja waliohudhuria katika mnada huo walibidi kadri ya uwezo wao, lakini bei waliyofika hailingani na bei elekezi waliyopewa na TRA na kupelekea kushindwa kuuza makontena hayo.

Kevela amesema kuwa, kampuni hiyo inasubiri muongozo kutoka kwa TRA kama inaweza kubadili bei ya kontena hizo.

“Tumekuja hapa kwa ajili ya kuuza vitu mbalimbali, wateja wamebidi kadiri ya uwezo wao, hatukuuza samani peke yake, lakini kontena bado hazijafika bei, tunasubiri watu wa TRA watupe muongozo zaidi, kwa maana mmeona watu wamefika milioni 20 hadi 30 lakini bei haijafika, unapouza mali za serikali lazima tunakuwa na bei elekezi, huwezi ukauza bei tofauti,” amesema.

Akizungumza katika mnada huo, mteja aliyejitaja kwa jina la Juma, amesema bei ya kontena hizo iko juu ukilinganisha na thamani ya samani zilizomo ndani yake, huku mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kalonga alisema bei elekezi iko juu kana kwamba wahusika wamepanga kontena hizo zisinunuliwe.

“Nilikuwepo tangu mnada uliopita, vitu viko bei juu, ushauri wangu TRA waangalie thamani ya vitu na waweke bei ambazo kila mtu ana uwezo wa kununua. Lakini bei waliyoweka ni ya kukomesha vitu visinunuliwe. Vitu vya thamani ya chini unaweka bei ya juu maana yake nini?” amehoji Kalonga.

Naye Fredy Mwandimele alilalamika ukubwa wa bei iliyopangwa na TRA akisema kuwa, kitendo cha ukubwa wa bei kitapelekea samani hizo kushindwa kununuliwa na kukaa muda mrefu bandarini hatimaye kuharibika, na kushauri TRA kuiachia kampuni ya Yono jukumu la kupanga bei ili kontena hizo ziuzwe.

“Bei zao ziko juu, minada mingi wananchi wanashindwa kumudu, minada inatakiwa mtu akifika bei ya juu mtu anatakiwa apewe, mnada ukiaghirishwa muda mrefu vitu vinaoza, mtu akifika bei anapewa ndiyo minada tuliyozoea, TRA wana bei ya juu, hiyo kazi ya kupanga bei wangewaachia YONO, inaonekana wanawakatilia, watu wanakuja kwenye mnada lakini wanashindwa kwa sababu bei ya juu,” amesema Fredy.

Kutokana na wateja kushindwa kufika bei elekezi ya kontena hizo, mnada huo uliaghirishwa hadi Jumamosi ijayo ya terehe 15 Septemba mwaka huu.

error: Content is protected !!