October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fidia Kimara- Kibamba yatinga kwa mwanasheria mkuu

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakapotafsiri sheria ya barabara ya mwaka 1932 pamoja na Kanuni zake za mwaka 1955 na marekebisho yake Na. 13 ya mwaka 2009 kwamba wakazi wa Kimara – Kibamba waliobomolewa nyumba zao walipwe fidia, itatekeleza matakwa hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu …. (endelea).

Mwaka 2017/2018 nyumba za wananchi zilizokuwa pembezoni mwa barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kibamba zilibomolewa bila kulipwa fidia.

Akijibu swali la Mbunge wa Kibamba, Issa Jumanne Mtemvu (CCM), leo tarehe 14 Februari, 2022 bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi – Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema sheria itakapotamka kwa mara ya mwisho haki itatolewa.

Katika swali la msingi, Mtemvu ameuliza Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutatua mgogoro wa bomoa bomoa wa nyumba za wananchi zilizokuwa pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kibamba mwaka 2017/2018.

Aidha, katika maswali ya nyongeza Mtemvu amesema kuna kesi ya ardhi chini ya Jaji Bongoyo mwaka 2005 ambayo ilihukumiwa mwaka 2013 ambapo kwenye dhamana hiyo wadai walihalalishwa eneo hilo ni la kwao na kama serikali inalihitaji ilitakiwa kulipa fidia.

“Kwa kuwa sheria hii ya barabara ya mwaka 1932, inakinzana na sheria nyingine ikiwamo ya vijijini ya mwaka 1999 ambayo ilifuta mikataba na sheria nyingine kwa kuwamilikisha watu ardhi serikali haioni haya ya kuondoa ukinzani huo? Amehoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri huyo wa Ujenzi amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam iliondosha nyumba na mali za watu zilizokuwa zimejengwa kinyume cha Sheria ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kibamba ikiwa ni maandalizi ya kupanua barabara hiyo toka njia mbili hadi njia nane ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo.

Amesema kulingana na Sheria ya Barabara ya Mwaka 1932 pamoja na Kanuni zake za mwaka 1955 na marekebisho yake Na. 13 ya mwaka 2009, imeainishwa kwamba upana wa hifadhi ya barabara hiyo kuanzia Kimara Stop Over hadi Kibaha (TAMCO) ni mita 121 kutoka katikati ya barabara kila upande.

“Hivyo, nyumba na mali zote zilizokuwa ndani ya eneo hili walikuwa wako ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kinyume na Sheria.

“Zoezi la kuwaondoa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha utekelezajiwa mradi huu lilifanyika kwa kufuata Sheria ya barabara na hadi sasa Serikali haina mgogoro wowote na wananchi walioondolewa ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.

Amesema endapo kutatokea mgogoro kati ya wananchi wa eneo la Kimara hadi Kibamba kuhusiana na bomoa bomoa wa nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro kinyume na Sheria, mgogoro huo utatatuliwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Aidha ameongeza kuwa kesi iliyozungumzwa na Mtemvu ipo kwa wakili mkuu wa serikali, ambaye yupo chini ya ofisi ya mwanasheria mkuu wa kiserikali.

“Hatua waliyochukua wananchi hawa kwenye vyombo vya kisheria ni sahihi na ninaomba nimhakikishie kwamba sheria itakapotamka kwa mara ya mwisho haki itatolewa,” amesema.

Kuhusu sheria ya barabara kukinzani, Kasekenya amesema wizara itaangalia kama kuna sheria za barabara zinazokinzana.

error: Content is protected !!