May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fedha za sherehe za Muungano kugawanywa

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Spread the love

 

RAIS wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, ameagiza fedha zilizopangwa kufanya sherehe za maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, zitumike kwa ajili ya shughuli za maendeleo Bara na Visiwani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu tarehe 26 Aprili 2021, na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya muungano huo, lililofanyika jijini Dodoma.

“Kwa busara za Mama yetu Samia, baada ya kufanya uamuzi kwamba mwaka huu tuadhimishe muungano wetu kwa kufanya kongamano, ameagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za muungano, zitagwanywa kwenda pande mbili za muungano,” amesema Dk. Mpango.

Hata hivyo, makamu huyo wa rais hakutaja kiasi cha fedha zilizopangwa kwa ajili ya kutekeleza sherehe hizo, ambazo zitagawanywa Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo.

“Kila upande utaamua kutumia hizo fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo,” amesema Dk. Mpango.

 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kusitisha sherehe hizo, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam.

Kiongozi huyo aliyefariki kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, mwili wake ulizikwa tarehe 26 Machi 2021, nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

“Imekuwa ni utamaduni wetu kuadhimisha sherehe za muungano kitaifa kwa gwaride maalumu na burudani, katika uwanja mahsusi.

“Kwa mwaka huu, kutokana na tukio la karibuni ambapo nchi yetu iliondokewa na kiongozi muhimu, tuliamua kwamba badala ya sherehe, tuadhimishe kwa kuwa na kongamano,” amesema Dk. Mpango.

error: Content is protected !!