FEDHA za misaada zinazotarajiwa kutolewa kwenye bajeti ya 2024/25, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zimepungua kwa asilimia 38, ikilinganishwa na Sh. 1.11 trilioni, zilizoahidiwa 2023/24. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Akiwasilisha mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya 2024/25, leo tarehe 6 Novemba 2023, bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema sababu za upungufu huo ni athari za ugonjwa wa UVIKO-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine, vilivyoathiri uchumi wa nchi za Ulaya ambazo ni watoaji wakubwa wa misaada.
Dk. Mwigulu amesema, katika bajeti ya 2024/25, Serikali inatarajia kukopa Sh. 12.29 trilioni, kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kuziba nakisi ya bajeti. Sh. 6.14 trilioni inatarajiwa kukopwa ndani ambapo Sh. 3.91 trilioni, inatarajiwa kulipa mikopoitakayoiva na Sh. 2.22 trilioni kwa ajili ya kuziba nakisi ya bajeti.
“Katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea kukopa kutoka vyanzo vya ndani kwa kiwango kisichozidi asilimia 1.0 ya Pato la Taifa kwa mwaka ili kutoathiri upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi,” amesema Dk. Mwigulu.
Kuhusu mikopo nje ya nchi, Dk. Mwigulu amesema Serikali inatarajia kukopa Sh. 6.15 trilioni, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu Sh. 3.60 trilioni na mikopo yenye masharti ya kibiashara Sh. 1.55 trilioni.
“Katika mwaka 2024/25, matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh. bilioni 47,424.9 (Sh. 47.42 trilioni). Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali Sh. bilioni 12,101.2 (Sh. 12.10 trilioni), mishahara Sh. bilioni 11,774.8 (Sh. 11.77 trilioni)na uendeshaji wa shughuli za Serikali Sh. bilioni 8,223.8 (Sh. 8.22 trilioni). Aidha, matumizi kwa ajili ya programu na miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 15,325.1 (Sh. 15.32 trilioni)ikijumuisha ruzuku ya maendeleo,” amesema Dk. Mwigulu.
Leave a comment