June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fedha za CCM zavuruga vyama Z’bar

Spread the love

FEDHA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinatumika kuvuruga mwelekeo na msimamo wa vyama vya upinzani visiwani Zanzibar, anaandika Regina Mkonde.

Kazi hiyo inafanywa kwa ustadi mkubwa na maofisa wa CCM visiwani humo kwa kushirikiana na maofisa wa Bara ili kuhakikisha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inapata uhalali wa kuendesha uchaguzi huo ambao umegubikwa na utata wa kikatiba na hata kugomewa na vyama, taasisi na wanataaluma nchini.

Fedha hizo zinachomekwa katika vyama ambavyo vinaonekana kutokuwa na msimamo wa pamoja ambapo Chama Cha National Reconstruction Alliance (NRA) pamoja na Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) vimekumbwa na mtikisiko wa fedha hizo. Tayari vyama 10 vimejinasua kwenye mtego huo.

Wakati Said Miraji, Mwenyekiti wa ADC akienda mbio kuokoa dhoruba ya fedha za CCM kuvuruga msimamo wa chama hicho wa kutoshiriki uchaguzi Zanzibar, kauli tata zimeendelea kuibuka ndani ya NRA.

Ni siku mbili zimepita baada ya aliyekuwa mgombea urais wa NRA, Seif Ali Iddi aliyeongozana na Suleiman Mohamed Gaddafi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kutoa tamko la kutoshiriki kwenye uchaguzi huo, baadhi ya viongozi wa NRA leo wameibuka na kukanusha tamko hilo kwa kudai “ni tamko la mgombea na si la chama.’

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Maelezo jijini Dar es Salaam, Hassan Kisabya Almas, Katibu Mkuu-Bara na bodi ya chama hicho wameeleza kwamba, tamko la mgombea wao halina baraka zao.

“Kujitoa kwake kwetu si hoja, lakini sifa zote hizo haziwezi kukitoa chama katika jambo lolote ikiwa chama kimeamua,” amesema Almasi huku akiongeza kuwa, watajiaminisha kuwa mgombea wao ama amehama chama au amefariki.

MwanaHalisi Online ilimtafuta mgombea huyo (Iddi) na kumuuliza juu ya tuhuma za baadhi ya viongozi wa chama chake kutokana na kutangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo uliotangazwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

Iddi amejibu, “tulikaa kikao tarehe 6 Januari mwaka huu na mwenyekiti wa chama na katibu tukaafikiana kutoshiriki kwenye uchaguzi wa marudio, viongozi wa bodi waliojitokeza leo wamenunuliwa,” amesema.

Iddi amesema kuwa, yeye binafsi hakukubali kushiriki kwa sababu, ufutwaji na urudiwaji wa uchaguzi huo haukuzingatia sheria na katiba, huku akimtaja ofisa mmoja wa ngazi ya juu katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuhusika na harakati za kurubuni vyama vya siasa kwa maslahi ya CCM.

“Huyu (anamtaja jina) anahusika kuvirubuni vyama kwa masilahi yake binafsi, na hawa viongozi waliojitokeza leo hawana msimamo,” amesema Iddi.

Chama cha NRA ni miongozi mwa vyama 14 vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa Tarehe 25 Oktoba mwaka jana kwa nafasi ya Rais ambapo ZEC ilifuta uchaguzi huo siku tatu baadaye.

error: Content is protected !!