FATMA Karume, mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania amesema, hajazaliwa kwa ajili ya kufanya kazi mahakamani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Fatma ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 23 Septemba 2020 wakati anazungumza na MwanaHALISI Online kuhusu uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili Tanganyika kuagiza kuondolewa katika orodha ya mawakili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Kamati hiyo imechukua uamuzi huo baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za kukiuka maadili ya uwakili kwa kuishambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania.
Soma zaidi:-
Alipoulizwa amejipangaje kuhusu uamuzi huo, Fatma ambaye ni mtoto wa Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Zanzibar amejibu hajapanga kufanya kitu chochote kwani hakuzaliwa mahakamani wala uwakili.
“Sijapanga kufanya kitu, mimi sijazaliwa mahakamani wala uwakili haini define. Maisha yanaedelea,” ameeleza Fatma.
Kuhusu kukata rufaa juu ya uamuzi huo, Fatma aliyepata kuwa Rais wa TLS kati ya mwaka 2018/19 amesema hana mpango huo.
“Uhalali wa maamuzi si kutokata rufaa. Uhalali wa maamuzi ni maamuzi yenyewe, mantiki yake na ubora wake.”
Fatma aliyehudumu kwenye uwakili kwa zaidi ya miaka 20 amesema “nataka maamuzi hayo yabaki kwenye historia ili miaka 100 kutoka leo Watanzania waelewe tulikuwa na mahakama ya aina gani.”

Kwa upande wake Dk. Rugemeleza Nshala, Rais wa TLS amesema Fatma ana nafasi ya kukata rufaa juu ya maamuzi hayo.
Licha ya Fatma Karume, kuondolewa katika orodha ya Mawakili wa TLS, wakili huyo, anayo nafasi ya kufanya shughuli zake za uwakili nje ya mipaka ya Tanzania Bara.
Akifafanua hilo, Wakili Frederick Kihwelo, Mwanachama wa TLS amesema, Fatma hatoweza kufanya kazi za uwakili upande wa Tanzania Bara, lakini anaweza akaendelea kufanya kazi Zanzibar au nje ya Tanzania bara ambazo atasajiliwa kufanya kazi za uwakili.
Wakili Kihwelo ametoa ufafanuzi huo wakati anazungumza na MwanaHALISI Online.
“Kuhusu wakili kuwekwa katika orodha ya mawakili ina maana kuna database na lazima uwe na namba ya uwakili kwa mujibu wa sheria.”
“Lakini ukiondolewa ina maanisha huwezi kufanya kazi ya uwakili Tanzania bara, anaweza fanya Zanzibar kama mwanachama wa Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS),” amesema Wakili Kihwelo.
Wakili Kihwelo amesema “Fatma anaweza akafanya kazi nje ya nchi kama atasajiliwa katika orodha ya vyama vya mawakili katika nchi husika.”
I don’t have a website