Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Fatma Karume aivuruga Mahakama
Habari za Siasa

Fatma Karume aivuruga Mahakama

Spread the love

MHIMILI wa Mahakama nchini, “umenajisiwa.” Kwa mara ya kwanza katika historia yake, chombo hicho kikuu katika utoaji haki kwenye Jamhuri ya Muungano, kimegoma kupokea hotuba ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea). 

Taarifa kutoka ndani ya TLS zinasema, chama hicho kimeshindwa kusoma hotuba yake, katika siku ya leo ya uzinduzi wa “Siku ya Sheria,” kwa kuwa wamekataliwa na Mahakama.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo TLS na Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, umekuwa ni utaratibu wa mhimili huo, miaka nenda rudi, kutoa nafasi kwa Rais wa TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambao ni wadau wakubwa wa mahakama, kuhutubia katika siku hii.

“Tulishaanda hotuba yetu na tukaiwasilisha kwa uongozi wa Mahakama  kwa ajili ya kuipitia. Lakini katika hali ambayo hatukuitarajia, tumenyimwa fursa hiyo,” ameeleza wakili mmoja wa kujitegemea ambaye hakupenda kutajwa jina.

Amesema, “tumeshafika pabaya sana. Mhimili huu unaonekana umeingiliwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu taifa hili lipate uhuru. Kama mahakama imeamua kufunga ndoa na serikali, watu watakwenda wapi.”

Aidha, kwa mara ya kwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania (JM), Prof. Ibrahim, Juma, amegoma hata kutambua uwapo wa kisheria wa TLS kwenye hotuba yake aliyoitoa muda mfupi kabla ya Rais Joh Magufuli, kuhutubia hadhira hiyo.

Rais wa TLS kwa sasa, ni Fatma Karume, mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na mjukuu wa muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 12 Januari 1964 na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Abeid Amani Karume.

Fatma alichukua nafasi hiyo, kutoka kwa Tundu Lissu, mbunge wa upinzani na mwanasheria machachari nchini.

Katika kipindi cha uongozi wake, sherehe za “Siku ya Sheria,” zilighairishwa mara kadhaa baada ya Lissu kugoma kufuta baadhi ya maneno yaliyokuwamo kwenye hotuba yake.

Haikuweza kujulikana mara moja, iwapo Fatma naye alitakiwa kuondoa sehemu ya maneno kwenye hotuba yake.

Ifuatayo hapa chini ni sehemu ya hotuba  ya Karume ambayo alikuwa aisome leo, tarehe 06 Februari  2019, jijini Dar es Salaam.

TANGU utotoni  nimefundishwa kwamba  vilivyokuwemo  kwenye mkoba wa  mwanamke  ni siri  yake. Bibi,  Mama au  Shangazi akikutuma  kumletea mkoba  wake,  kwetu ilikua  marufuku kuchungulia  ndani.

Leo, nitaivunja  miiko  kwa kuwaeleza  vichache ninavyobeba  kwenye  mkoba wangu:    miwani,  maana sioni  vizuri, rangi  ya mdomo  hii  ni muhimu,  kipepeo,  Dar kuna  joto  kali, na wanaonijua  vizuri  wanafahamu ukikuta  pesa  kwenye Mkoba  wangu ni  bahati.

Lakini  sitoki  bila ya  kubeba  Katiba ya  Jamhuri  ya Muungano wa  Tanzania.    Sitaweza kugawa  kila  kilichopo ndani  ya mkoba  isipokua matamshi  ya  Katiba. Na  ningependa  kuanza hotuba yangu  kwa  kuwakumbusha Utangulizi  na  Misingi ya  Katiba  yetu. Katiba inaanza na utangulizi  ufuatao:

“Kwa  kuwa  sisi wananchi  wa  Jamhuri ya  Muungano  wa Tanzania   tumeamua  rasmi  na kwa  dhati  kujenga katika  nchi yetu,  jamii inayozingatia  misingi  ya UHURU,  HAKI,  UDUGU na AMANI: Na  kwa  kuwa misingi  hiyo  yaweza tu  kutekelezwa  katika jamii yenye  demokrasia  ambayo serikali  yake  husimamiwa na  Bunge lenye  wajumbe waliochaguliwa  na  linalowawakilisha  wananchi, na pia  yenye  Mahakama huru  zinazotekeleza  wajibu wa  kutoa haki  bila woga  wala  upendeleo wowote,  na  hivyo kuhakikisha kwamba  haki  zote za  binadamu  zinadumishwa na  kulindwa,  na wajibu wa  kila  mtu unatekelezwa  kwa uaminifu.

“Kwa  hiyo  basi, Katiba  hii  imetungwa na  Bunge  Maalum la Jamhuri  ya  Muungano wa  Tanzania,  kwa niaba  ya  Wananchi, kwa madhumuni  ya  kujenga jamii  kama  hiyo, na  pia  kwa ajili  ya kuhakikisha  kwamba Tanzania  inaongozwa  na Serikali  yenye kufuata  misingi ya  Demokrasia na  Ujamaa.  “Misingi  ya  Katiba yetu  ni  UHURU, HAKI,  UDUGU,  AMANI, DEMOKRASIA  NA UJAMAA.

Ni  muhimu  pia kutambua  kuwa  neno Demokrasia  limetajwa mara  mbili  katika utangulizi  huu.  Na waliotunga Katiba  walielewa  kwamba Mahakama  huru  inayotoa haki bila  woga  wala upendeleo  wowote  ina hakikisha  haki  zote za binadamu  zinadumishwa  na kulindwa  na  ina umuhimu  wa  pekee kwenye kulinda  misingi  ya katiba.

Nimeelezwa  kwamba  uongozi wa  Mahakama  umeamua kauli  mbiu ya  mwaka huu  kuwa  ni :  “Utoaji  wa Haki  kwa  Wakati: Wajibu  wa Mahakama  na Wadau”, na nimeambiwa nijikite kwenye mada hiyo. Nitaanza  na  Wajibu wa  Mahakama  na nitamalizia  na  wajibu wa wadau.

Wajibu  wa Mahakama

Wajibu wa  Mahakama umewekwa wazi  kwenye  Katiba yetu.  Ibara 107A  (1) inasema, “Mamlaka  yenye kauli  ya  mwisho ya  utowaji  haki katika  Jamhuri  ya Muungano itakuwa  ni Mahakama.”

Ibara ya 107A(2)(b) ya Katiba inaeleza,   “Katika  kutoa uamuzi  wa  mashauri ya  madai  na jinai  kwa  kuzingatia sheria,  Mahakama zitafuata  kanuni zifuatazo,  yaani- a) Kutenda  haki  kwa wote  bila  ya kujali  Hali  ya mtu,  kijamii  au kiuchumi; b)  kutochelewesha  haki bila  sababu  ya kimsingi; c)  kutoa  fidia ipasavyo  kwa  watu wanaoathirika  kutokana  na makosa ya  watu  wengine, na  kwa  mujibu wa  sheria  mahususi ilioyotungwa  na Bunge; d)  kukuza  na kuendeleza  usuluhishi  baina ya  wanaohusika  katika migogoro.   e) kutenda  haki  bila ya  kufungwa  kupita kiasi  na  masharti ya kiufundi  yanayoweza  kukwamisha haki kutendeka.”

Ibara 107B  “Katika  kutekeleza mamlaka  ya  utoaji haki,  mahakama  zote zitakuwa huru  na  zitalazimika kuzingatia  tu  masharti ya  Katiba  na yale ya  sheria  za nchi.” Kwa hiyo wajibu wa Mahakama ni kutoa HAKI.

Mahakama  inatekeleza  majukumu yake kama yalivyotajwa  kwenye Ibara ya 107(A) ya  Katiba  yetu, inatakiwa  kutoa HAKI;  kutochelewesha  utoaji wa  Haki  bila  ya  sababu ya  kimsingi  na  (kutenda  haki bila  kufungwa  kupita kiasi  na  masharti ya  kiufundi yanayoweza  kukwamisha haki  kutendeka.

Majukumu  ya  Mahakama yetu  kwa  mujibu wa  Katiba  yetu ni  utoaji wa  HAKI na  si  USIKILIZAJI wa  kesi  tu.

Haki ya  kusikilizwa  kesi yako  ina  madhumuni ya  kuhakikisha  kuwa unapata USAWA  MBELE  YA SHERIA  na  si kuhakikisha  unapata  HAKI mbele  ya sheria.    Haki inapatikana  pale  Mahakama itaendeshwa  na  watu wenye uwezo,  uzoefu,  weledi, maadili,  uhuru  wa fikra,  ambao hawana  uoga na  wanaoheshimu  matakwa ya  Katiba  yetu.   Kusikiliza kesi  na  kutoa maumuzi  ni  rahisi sana,  na  kila mtu  anaweza  kufanya hivyo.

Lakini  kusikiliza  kesi na  kutoa  maamuzi ya  haki  ni vigumu maana  inahitaji,  KNOWLEDGE, EXPERIENCE,  INDEPENDENCE,  A SENSE OF  DUTY,  A CALLING  AND  FEARLESSNESS. Haki  za  wananchi si usikilizwaji  wa  kesi zao  tu  na haki  ya  kukata rufaa  kwa   maana kesi inaweza  kusikilizwa,  kesi  inaweza kukatiwa  rufaa  bila ya  HAKI kutendeka.    Kwa mujibu  wa  katiba yetu  majukumu  ya Mahakama  ni UTOAJI  WA HAKI  KWA  WAKATI.

Huwezi  ukawa  mwoga na  hapo  hapo ukatoa Haki. Huwezi  ukaweka  mbele maslahi  yako  na ukatoa  Haki.  Utabaki na woga  tu lakini  Haki (Justice)  itakua ndoto. Ili  tuelewe umuhimu  wa  Katiba ningependa  kutoa  mfano mdogo  tu.  Kwenye ujenzi  wa  Standard Gauge  Railway,  vipimo baina  ya  vyuma vya reli  vitabaki  4ft 8  ½  inch au  1,435  mm kutoka  Dar  mpaka Rwanda. Hii  haiwezi kubadilika  hata  kama reli  inapanda  au kushuka mlima. Lakini mabehewa  yanaweza  kubadilika.

Unaweza  kuwa  na behewa la  kubeba  mizigo, behewa  la  kubeba wanyama,  behewa  la kubeba mafuta,  behewa  la kubeba  watu  daraja la  kwanza  na behewa la kubeba  watu  daraja la  mwisho  ilimradi magurudumu  ya mabehewa  ni ya  kutembea  kwenye reli  ya  standard gauge. Ukiweka behewa  lenye  magurudumu makubwa  au  madogo kuliko  ya  standard gauge,  behewa litapinduka  na  watu watajehuriwa.    Ili standard  gauge ifanye  kazi ipasavyo,  lazima  magurudumu ya  mabehewa  yote yafuate muundo  wa standard gauge. Kwamba Mahakama  lazima  ijitathmini yenyewe. Ijiulize  mara  kwa mara,  kweli  tunafuata Katiba  ipasavyo?

Nisingependa  kumaliza  bila ya  kugusia  uendeshaji wa  kesi  za jinai Tanzania.    Sisi  Wanasheria tunaona  huzuni  sana namna  criminal justice  system inavyotumiwa  kuonea  na  si  kuendesha mashitaka dhidi  ya  watuhumiwa.   Watu  wanakamatwa  na wanawekwa  ndani bila  ya dhamana  wakati  upelelezi wa  kesi  haujakamilika. Nina maswali  mawili tu  ya  kuuliza:

Kama  upelelezi  haujakamilika unauhakika  gani kwamba  huyu  mtu ana  kesi  ya kujibu?    Kama nitaendelea  na mfano  wangu  wa Standard  Gauge,  Katiba yetu  ya 1977  na mabadiliko  yote  yaliyofanywa kwenye  Katiba  hii  ni  Kama mfumo mpya  wa  reli. Tujiulize  kweli kukamata  watu  na kuwaweka ndani  bila  ya haki  ya  dhamana ni  jambo  linaloweza kuvumiliwa kwenye  mfumo  wa Katiba  yetu  yenye Bill  of  Rights?

Lingekuwa behewa,  hili  ni la  Standard  Gauge au  tumeliacha  behewa lililoundwa kutembea  kwenye  reli nyingine  litembee  kwenye reli  yetu  na kila likitembea  linaathiri  wananchi?   Tujikumbushe  kwamba  non-bailable offences  zilikuwepo kwa  capital  offences only  hata  kabla ya  Katiba  ya 1977 ninayoifananisha  na  ujengaji wa  Standard  Gauge ya  Katiba yetu.

Katiba  yetu  imetambua haki  na  wajibu muhimu  wa  wananchi (Bill  of Rights),  chakusikitisha  ni kwamba  badala  ya makosa yaliyokuwa  hayana  dhamana kupunguzwa,  yanazidi  kuongezeka kadri  siku zinavyokwenda  japokuwa  Haki na  wajibu  Muhimu wa wananchi  bado  unatambulika na  Katiba  yetu. Tumefika  mahala ambapo  makosa ya  kutolipa  kodi yanakuwa  predicate  offences kwa makosa  ya  utakatishaji wa  pesa  ambayo hayana  dhamana.  Kwa hiyo mtu  akishutumiwa  kutokulipa kodi  anaweza  wekwa ndani  bila dhamana  kwa kosa  la  utakatishaji wa  pesa.

Na  ataswekwa  ndani mpaka pale  D.P.P  atakapoamua kukamilisha  upelelezi  na kuendelea na  kesi.    Wakati haya  yanatokea,  tumesahau kwamba,  huyu “mtuhumiwa”  ana watoto,  ana  mke, ana  wazazi,  ana ndugu  na  wote wanamtegemea  yeye.   Siku  D.P.P  akiamua hataki  kuendelea  na kesi, “mtuhumiwa”  ana i tolewa  bila ya  fidia.    Ninajiuliza kweli  hii  ni HAKI iliyodhamiriwa  na  Katiba yetu?   Kwa  fikra zangu,  Hapana,  hapana na hapana  tena.

Kama  nilivyosema  awali kazi  ya  Mahakama ni  kuhakikisha  Haki inatolewa  kwa muda  muafaka  na kwa  kuzingatia  misingi ya  katiba hasa  Haki na  Wajibu  Muhimu wa  wananchi.  Tusikae tukamlaumu DPP  tu,  maana yeye  hana  wajibu wa  kikatiba  kutoa HAKI.  Wajibu  huo ni wa  Mahakama.

Kwa  hivyo  akishitaki watu  wakati  upelelezi haujakamilika,  akifuta mashitaka  baada  ya mtu  kukaa  maabusu kwa miaka  6  akaamuru akamatwe  tena  pale pale  Mahakamani,  tunaweza kumlaumu  kwa kutokufuata  maadili  ya Waendesha  mashtaka,  lakini sisi sote  kama  wananchi, including  DPP  mwenyewe, tunategemea Mahakama  itende  HAKI na  hakuna  muhimili mwingine  utakao  pata lawama isipokuwa  Mahakama maana ibara 107A  (1) inasema, “Mamlaka  yenye kauli  ya  mwisho ya  utowaji  haki katika  jamhuri  ya muungano itakuwa ni  Mahakama”.

Na wajibu huu haukwepeki. Ninakwenda  Segerea mara  kwa  mara na  ninataka  kuwaambia, December  2018, kulikua  na  watu walioko  gerezani  wanaume ni   1,723,  kati ya  hao  waliofungwa kwa  mujibu  ya hukumu  ya Mahakama  walikuwa 158  tu  na walioko  rumande  ni 1,565.    Upande wa  wanawake kulikuwa  na  walioko gerezani 313,  waliofungwa  baada ya kesi  zao  kusikilizwa walikua  66  na walioko  rumande  ni 247.    Hiyo ndio hali  halisi ya utoaji  wa HAKI  kwa upande wa kesi za jinai.

Ningependa  kumalizia na  ki-joke kimoja, dada  yangu  mpendwa Balozi Mwanaidi  Maajar anapenda  kuniambia mara kwa mara. Siku  moja  Tembo huko  Serengeti  kamuona Paa  anakimbia  kweli huku akichungulia  nyuma  kila baada  ya  hatua chache. Tembo akamsimamisha Paa  akamuuliza  “Kulikoni? Mbona  unakimbia  kama unafukuzwa?” Paa  akamjibu huku  anahema  “Nasikia wanatafuta mbuzi  kwa  kosa la  money  laundering”.

Tembo  kamtizama  Paa kwa mshangao  mkubwa  akasema “Sasa  wewe  Paa unakimbia  nini?  Hujijui kwamba  wewe ni  Paa  sio Mbuzi?”    Paa  akamtizama Tembo  kama  vile mjinga kweli  akamjibu  “Mimi ninajijua  kwamba  mimi ni  Paa,  wewe pia unajua  kwamba  mimi ni  Paa,  lakini hao  wanaotafuta  mbuzi wanajua mimi  ni  Paa?   Na  kama  hawajui itanichukua  miaka  20 kuthibitisha  mahakamani kuwa  mimi  ni Paa  na  Siyani mbuzi.    Sina muda  huo”.

Alivyomaliza  kusema  akaendelea kukimbia  kama anakimbizwa  na ibilisi.    Baada  ya muda  Paa  akatizama nyuma akamkuta Tembo  naye  anakimbia kama anafuatwa na  Israeli. Wajibu  wa Wadau Sasa  ninataka kusema  wajibu  wa wadau.  Ninachukuwa  fursa hii kuwakumbusha  wananchi  wajibu wao  ndani  ya Ibara  ya  26 inayosema kama ifuatavyo:

(1)  “Kila  mtu ana  wajibu  wa kufuata  na  kuitii Katiba  hii  na sheria  za Jamhuri  ya Muungano. (2)    “Kila mtu  ana  haki, kwa  kufuata  utaratibu uliowekwa  na sheria,  kuchukua hatua  za  kisheria kuhakikisha  hifadhi  ya Katiba na  sheria za nchi”.

Ni  wajibu  wetu sote  kufuata  na kuitii  Katiba  na kuhakikisha  hifadhi  ya Katiba yetu.    Na  ni wajibu  wetu  sote kuilinda  Katiba  yetu na  sheria zetu. Ninataka  kumaliza kwa  kumnukuu  Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere  kotoka Hotuba yake “Nyufa” “Hatuwezi  kuendelea  kupuuza Katiba,  ndiyo  sheria ya  msingi; sheria  nyingine zote  zinatokana  na Katiba.

Haiwezi  kupuuzwa  na hatuwezi kuendela  na  uatratibu wa  kupuuza  Katiba ya  nchi  yetu au kuwa  na  Rais anayeonea  haya  kuitetea Katiba  naye  amechaguliwa kwa  mujibu wa  Katiba,  ameapa kuilinda  Katiba  hiyo halafu  anona haya  hawezi kuitetea  Katiba  hiyo.   Mtu  ambaye  kawezi kuitetea Katiba  ya  nchi yetu,  hawezi  kuilinda, hawezi  kuisimamia  baada ya kiapo, hatufai.   Hafai!”

Ahsanteni.

Fatma Amani  Karume President  of the Tanganyika Law Society 2018  – 2019 Dar  es Salaam, 1st  February 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!