December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bashiru ‘ashughulikiwa’

Spread the love

KAULI ya Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwamba chama kinachoondoka madarakani wakati kina dola ni uzembe, imetibua wengi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Fatma Karume, mwanaharakati na mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Aman Karume amesema chama chenye wazo la kutumia dola kushika madaraka sio chama ni kikundi cha wahuni.

Amesema, Dk. Bashiru anapaswa kuachana na mawazo ya kale na kwamba afute kauli hiyo.

“Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru anasema CCM itahakikisha inaendelea kushika dola. Dola ni Serikali, Mahakama na Bunge. Dola ni Taifa, chama cha siasa si dola.

“Ukiona chama kinang’ang’ania kushika dola, hicho sio chama cha siasa ni kikundi cha wahuni kisicho na nia njema na taifa,” amesema Fatma.

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT-Wazalendo leo tarehe 9 Machi 2020, jijini Dar es Salaam, Fatma amesema kazi ya CCM ni kuisimamia serikali, na si kushika dola.

Kutokana na kauli ya Dk. Bashiru, Fatma amewataka vijana wa ngome hiyo, kutokuwa na tamaa ya kutumia dola kwa ajili ya kubaki madarakani, bali kuwa na sera zinazovutia wananchi watakaowaweka madarakani.

“Nafikiri Tanzania tumepata mkanganyiko sana kuhusu sheria, siku za karibuni kumetokea taharuki CCM imeshika dola na itatumia dola kuhakikisha inashika serikali.
“Nyinyi mnataka siku moja mshike serikali, nataka nianze kukuelewesheni, msitamani hata siku moja kushika dola, dola sio yenu,” amesema Fatma na kuongeza:

“Chama cha siasa kazi yake ni kuendesha serikali kwa mujibu wa Sheria na Katiba, unakwenda na sera zako kujenga mahusiano baina ya chama cha siasa na wananchi. Chama kazi yake kutubembeleza kutuambia maneno mazuri tuwape kura, chama cha siasa kazi yake si kutisha.”

Akizungumza na Kampuni ya Habari ya IPP tarehe 6 Machi 2020, Dk. Bashiru alisema, chama kilichopo madarakani kikishindwa kutumia dola kubaki madarakani, huo unakuwa uzembe wao, akitolea mfano wa uzembe uliofanywa na Chama cha KANU cha nchini Kenya na Unip cha Msumbiji.

error: Content is protected !!