December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fastjet, serikali sasa hapatoshi

Spread the love

SIRI kuu juu ya kampuni ya ndege ya Fastjet, kusitisha shughuli zake za usafirishaji wa abiria nchini, imefichuka. Anaripoti Regina Mkonde …. (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya serikali zinasema, mamlaka nchini Tanzania zimelazimika kuizua kampuni hiyo, kutoa huduma za kusafirisha abiria, kutokana na kukabiliwa na mzigo wa madeni kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) na watoa huduma wengine.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo tarehe 27 Desemba 2018, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Hamza Johar amesema, Fastjet haitaruhusiwa kusafirisha abiria nchini, hadi pale itakathibitisha uimara wake.

Aidha, Johar amesema, serikali itaendelea kuzishikilia ndege za kampuni ya Fastjet hadi itakapoweza kumaliza kulipa madeni yake.

Serikali inadai kuwa kampuni ya Fastjet inadaiwa mamilioni ya shilingi na TCAA na watoa huduma wengine wa usafiri wa anga.

“Fastjet ana madeni makubwa. Anadaiwa na mkodishaji (mwenye ndege). Huyo mkodishaji (mwenye ndege zake), anaomba ndege hizo zirudi kwake, kwa maana ziondoke nchini,” anaeleza.

Anasema, “lakini sisi kama mamlaka ya usafiri wa anga tukasema, haziwezi kuondoka kwa sababu zina madeni makubwa.”

Anaongeza, “ndege hizi haziwezi kuondoka. Ni ndege za kitanzania zina usajili wetu. Nikiwa kama mkurugenzi mkuu, nina mamlaka ya kusema ndege hii isiondoke; na haitaondoka mpaka madeni haya yalipwe.”

Mkurugenzi huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa tayari Fastjet wameondosha ndege yao moja kwa hila; jambo ambalo limeilazimisha mamlaka yake kuzing’ang’ania hizo zilizobaki.

Kwa mujibu wa Johar, kuna ndege moja ya Fastjet ambayo wakurugenzi wake walisema, inakwenda kwenye matengenezo, kumbe wamekwenda kuificha Nairobi.

Hata hivyo, Johar anasema, “lakini hata kama iko Nairobi, mwenye mamlaka wa kuufuta usajili wa Tanzania, ni mkurugenzi TCAA na sheria inasema hatutafuta usajili wetu mpaka madeni yote yatakapolipwa.”

Johari amekana madai yaliyotolewa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii, kuwa hatua ya mamlaka yake kuzuia Fastjet kuendelea na shughuli zake, inalenga kuibeba kampuni ya ndege ya taifa – Air Tanzania Company Limited (ATCL).

Kauli ya mkurugenzi huyo, imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet nchini, Lawrence Masha, kuituhumu serikali kuihujumu kampuni hiyo.

Masha ambaye alipata kuwa waziri katika serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete amesema, mamlaka hiyo imezuia kampuni yake kuingiza ndege yake iliyonunua kwa ajili ya kuifufua kampuni hiyo, lakini serikali imekuwa ikiwawekea ngumu.

Alidai kuwa kisingizio ambacho serikali inakieleza cha kuwa kampuni inadaiwa, hakina maana yeyote.

“Hakuna asiyedaiwa. Hata ATCL ambayo imenunua ndege kwa fedha za walipa kodi na kwa kutumia utaratibu wa keshi, bado inadaiwa. Hata serikali yenyewe inadaiwa,” amesisitiza Masha.

Wakati Johar akikana madai ya kuibeba ATCL, waziri wa mawasiliano na uchukuzi, mhandisi Isack Kamwelwe, amewahi kunukuliwa akisema, serikali itailinda ATCL bila kigugumizi.

“Hawa Fastjet, walitubipu. Tumewapigia. Tumewazuia kurusha ndege zao na tayari tumeagiza ATCL kurusha ndege katika maeneo yote ambayo Fastjet walikuwa wanakwenda,” alieleza mhandisi Kamwelwe.

error: Content is protected !!