August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Farid Mussa sasa rasmi Hispania

Farid Mussa (20) wa klabu ya Azam FC (Kulia)

Spread the love

BAADA ya sintofahamu ya muda mrefu juu ya winga Farid Mussa (20) wa klabu ya Azam FC kwenda katika klabu ya Deportivo Tenefife ligi daraja la kwanza nchini Hispania kucheza soka la kulipwa, hatimaye kibali chake kufanyia kazi nchini humo kimeatikana, anaandika Kelvin Mwaipungu.

Farid amepinga taarifa kuwa uongozi wa klabu ya Azam umekwamisha safari yake ya kwenda kucheza soka la kimataifa.

“Napenda kumshukuru Mungu baada ya kupata visa, namshukuru pia Abdul (Mohamed), Meneja Mkuu wa Azam kwa kupigana hadi suala hili limekamilika, ninawaomba Watanzania wajue kuwa Azam haikuwa inanibania bali masuala ya visa yalikuwa yakisumbua ubalozini”. Amesema Farid.

Ameeleza kuwa, muda wowote kuanzia mwezi Januari ataenda kuanza maisha yake mapya ya soka la kulipwa kwenye klabu ya Deportivo Tenefife.

Jaffar Iddi, ofisa habari wa Azam FC amesema, “Uongozi wa Azam FC ulikuwa sambamba na Tenerife kuhakikisha Farid anaondoka, tunashukuru suala hilo limekamilika kwa asilimia 98. Mungu akijaalia ndani ya wiki mbili zijazo au wiki moja anaweza kuondoka hapa nchini kuelekea Hispania.”

Kilio cha wapenzi na mashabiki wa mchezo wa soka juu ya kuchelewa kwa nyota huyo kinatokana na idadi ndogo ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka nje ya nchi kama ilivyo kwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Nyota wengi wa Tanzania kucheza soka nje ya nchi inaweza kuleta manufaa kwa timu ya taifa hapo baadaye kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye uzoefu kimataifa.

error: Content is protected !!