Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Fao la kustaafu laitafuna serikali
Habari za SiasaTangulizi

Fao la kustaafu laitafuna serikali

Marehemu Mwalimu Samson Kasuku Bilago enzi wa uhai wake
Spread the love

CHOZI la aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Buyungu, Mwalimu Samson Kasuku Bilago, juu ya kiinua mgongo cha wafanyakazi wa umma, waliojiunga kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, bado linaendelea kuitafuna serikali. Anaripoti Jumbe Suleiman .… (endelea).

Mwalimu Bilango aliliambia Bunge mjini Dodoma, Februari mwaka huu kuwa hatua ya serikali ya kuamua vikokotoo vya wafanyakazi, ni jambo linaloweza kuingiza nchi kwenye mgogoro.

Alisema, “Bunge litakuwa linafanya makosa makubwa sana, iwapo itamuachia waziri mwenye dhamana na mifuko, kuamua hatima ya wafanyakazi. Hili ni jambo kubwa sana. Haliwezi kuachwa mikononi mwa watu wachache.”

Mwalimu Bilago alikuwa akichangia muswaada wa sheria uliyotaka kuungwanishwa kwa mifuko minne ya hifadhi ya Jamii.

Alisema, “ninaomba muswada huu ueleze kila kitu. Kutaka vikokotoo viwekwe kwenye kanuni, kunatoa mwanya kwa waziri kuja na mambo yake yasiyo na manufaa kwa wafanyakazi.”

Alisema, “tukienda kuficha kwenye kanuni mambo haya (vikokotoo), halileti afya. Tukikuta baada ya kufanya tathimini, kuwa hali zao ni mbovu tutarudi tena humu kuja kushughulikia hili? Wabunge tukubaliane tusipitishe sheria ambayo ni kimya.”

Alitaka pia vikokotoo vinavyopelekwa katika mifuko iliyounganishwa, vibaki kama vilivyo na uweke utaratibu upya kwa wanachama wanaojiunga baada ya sheria mpya kupitishwa.

Katika mkutano wake huo wa Februari mwaka huu, Bunge la Jamhuri, pamoja na mengine, liliruhusu kuundwa kwa mfuko mmoja wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Kuundwa kwa mfuko huo kulifuatia Bunge kuridhia mapendekezo ya serikali ya kuuganisha mifuko ya LAPF (Serikali za Mitaa); PSPF (watumishi wa Umma); watumishi wa Serikali Kuu (GEPF) na PPF kuwa mfuko.

Sekta binafsi ilibaki chini ya mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF).

Akipinga maoni ya Mwalimu Bilago, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, aliliambia Bunge kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), lilipeleka maombi ya kutaka wabunge wasiwaamulie kuhusu vikokotoo vya mafao yao.

Jenista alidai kuwa Tucta imetaka suala hilo liachwe mikononi mwao ili waliweke kwenye kanuni ambazo watashirikishwa katika kuzitunga.

Alisema, “hatua ya serikali ya kuunganisha mifuko hiyo, kunalenga kuboresha mafao ya wanachama na kuongeza mafao mapya yaliyokuwa yakihitajika sana na wanachama.”

Alisema, kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, ni kujibu kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi nchini.

Sakata juu ya “vikokotoo” limeibuka upya nje ya Bunge, hasa kwenye mitandao ya kijamii, kufuatia baadhi ya wafanyakazi waliostafu kujikuta wakiondoka ofisini wakiambulia patupu.

Akizungumzia suala hilo, aliyewahi kuwa katibu mkuu kwa miaka mingi katika ofisi ya rais (utumishi), Ruth Mollel anasema, “serikali imeamua kuwapunja wafanyakazi.”

Mollel ambaye sasa ni mbunge wa Viti Maalum (Chadema), anasema kuwa “…kikokotoo cha 1/540 kilikuwa ndani ya sheria. Lakini Bunge la wengi likakataa; na hivyo kutoa mwanya kwa serikali kudhulumu wafanyakazi.”

Anasema, “hatua ya serikali ya kutoa asimia 25 kwa mfanyakazi anayestaafu, kutasababisha fedha nyingi ambazo ni jasho la mfanyakazi kubaki mikononi mwa serikali.”

Anasema, “kufanya hivyo, kutazifanya familia za wafanyakazi kusukumwa kwenye lindi la umasikini na ufukara.”

Waziri wa maliasili na utalii, Dk. Hamis Kigwangala, anakiri katika ukurasa wake wa tweeter kuwa mjadala wa mafao ni mkubwa sana.

Anasema, “mjadala ni mkali sana na naona watu wanataka kujadiliana na serikali. Nashauri fuaeteni taratibu kupitia vyama vyenu vya wafanyakazi.

Zungumzeni na wahusika. Mtasikilizwa. Mimi sihusiki na kazi/ajira, mtanitoa macho bure.”

Katika ujumbe mwingine, Kigwangalla anasema, “baada ya kushambuliwa sana na kupitia maoni ya wengi hapa twitter na WhatsApp, nimeona hizi kelele si za kupuuzwa; ama vikokotoo hakijaeleweka vizuri au ushirikishwaji wadau haukuwa mpana ama kikokotoo kweli kina shida. Nimeongea na waziri husika, ameniarifu analishughulikia.”

Hata hivyo, akijibu madai hayo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, anaeleza kuwa mjadala unaoendelea kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, haielezi ukweli wa kilichotokea.

Anasema, “mijadala mingi inayoendelea, imelenga kuwapotosha kwa makusudi wanachama wa mifuko. Ukokotoaji huu, ulianza miaka minne iliyopita na tayari wafanyakazi wa NSSF (mfuko wa hifadhi ya jamii) na PPF (mfuko wa pensheni wa mashirika ya umma) wameanza kulipwa kupitia vikokoto hivyo.”

Alisema, “hatua ya kuunganisha mifuko hii ya pensheni kunalenga kupunguza gharama za uendeshaji kutoka asilimia 19 hadi asilimia tisa. Kutasaidia kuondoa ushindani usio na tija baina ya mifuko ya pensheni na kupunguza migogoro.”

Wimbo wa serikali uliibwa “mithili ya kasuku” na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Surukamba.

Akisoma maoni kamati yake, Serukamba alisema, mifuko yote mitano ilikuwa inatumia takribani Sh. 235.8 bilioni kwa mwaka kama gharama za uendeshaji.

Alidai kuwa bodi za wadhamini wa mifuko zilitumia kiasi cha Sh1.7 bilioni kwa kila mwaka kuhudumia wajumbe wake 45 kama posho na ada nyingine.

Serukamba ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) alisema, kamati yake imebaini kuwa matumizi ya fedha za menejimenti kwa wajumbe kwa ajili ya mishahara na stahili nyingine katika mifuko hiyo, ni makubwa na yalikuwa yanapanda kila mwaka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!