June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fahamu Shinikizo la Damu (2)

Mchoro unaonyesha madaraja ya shinikizo la damu

Spread the love

Aina za vipimo vya presha

KATIKA toleo la kwanza la safuu hii wiki iliyopita nilieleza aina mbili za shinikizo la damu. Nilisema aina ya kwanza ni shinikizo la damu la juu (hypertension) na aina ya pili ni shinikizo la damu la chini (hyportension). Vilevile, nilieleza madhara dalili pamoja na athari zitokanazo na ugonjwa wa hypertension. Leo nitaeleza vipimo vinavyotumika kujua ugonjwa huo.

Kiwango cha msumkumo wa damu kinapimwa kwa kifaa maalum kinachoitwa Mashine ya Kupima Msukumo wa Damu (Blood Pressure Machine/ BP, au kitaalam kinaitwa Sphygmomanometer).

Kifaa hiki majibu yake yanakuwa na namba mbili, na ni muhimu kuzifahamu ili kuweza kutafsiri na hivyo kutambua presha uliyonayo ina ukubwa gani.

Madaraja ya presha   Sistoliki (mmHg)              Diastoliki (mmHg) 

kawaida                                     <120                                     <80

Inayoelekea kupanda             120-139                                80-89

Presha hatua ya 1                    140-159                                90-99

Presha hatua ya 2                    160-179                              100-109

Presha hatua ya 3                     ≥180                                   ≥110

BP inasoma msukumo wa juu wa mzunguko wa damu na namba hizi huitwa msukumo wa ‘Sistoliki’ (systolic pressure) na  inatokea pale moyo unaposukuma damu kuisambaza mwilini.

Namba nyingine ya BP inaitwa msukumo wa ‘Dayastoliki’ (Diastolic Pressure) ambapo msukumo huu unanakiliwa wakati moyo umetulia baada ya kusukuma damu.

Kwa mfano, daktari wako au nesi akikuambia presha yako ni 140 chini ya  80 na inaandikwa 140/80mmHg, inamaana una Presha ya Sistoliki 140 na Presha ya Dayastoliki 80.

Kwa kawaida namba za juu zinakuwa kubwa, kwani ni wakati moyo unasukuma damu na kufanya shinikizo kwenye kuta za damu kuwa kubwa. Namba za chini zinakuwa ndogo kwani ni wakati ambapo shinikizo kwenye kuta za damu linakuwa dogo; moyo hupumzika kidogo kabla ya kusukuma damu kwa mara nyingine.

Kitabibu utakuwa umegundulika kuwa una presha ya kupanda (Hypertension) kama vipimo vinaonyesha umepima mfululizo si chini ya mara tatu mfululizo, kwa kipindi fulani, na vipimo vyote vikaonyesha presha bado ipo juu. Huwezi kupima mara moja na presha ikaonekana ipo juu ukasema una tatizo la presha ya kupanda.

 

Madaraja ya Presha

Presha ya Kawaida. Presha inakuwa ya kawaida kama itakuwa sio zaidi ya 120/80 mmHg.

Inayoelekea kuwa presha ya kupanda  (Pre-hypertension)

Hii ni presha iliyopanda kidogo zaidi ya presha ya kawaida, na ni kiwango ambacho bado kinaweza kikaonekana hakihitaji matibabu ya dawa, bali ni matibabu ya kuangaliwa maendeleo yake ikiwa ni pamoja na kupunguza ulaji wa chumvi na kufanya mazoezi ya kutosha. Daraja hili linaonyesha kuna dalili za mtu huyu kuweza kupata presha ya kupanda.

Katika presha hii, kipimo kitasoma kuanzia Sistoliki 120 mpaka 139 mmHg, au Diastoliki itaonyesha kati ya 80 mpaka 89 mmHg.

Hatua ya kwanza ya presha ya kupanda

Hatua ya kwanza ya presha ya kupanda ni pale sistoliki (mgandamizo wa juu) inapokuwa kuanzia 140 mpaka 159 mmHg au ni pale presha ya diastoliki inapofikia kati ya 90 mpaka 99.

 

Hatua ya pili ya presha ya kupanda

Hii ni hatua hatari, na inatokea pale sistoliki inapofikia 160 mmHg na zaidi au ni pale presha ya diastoliki inapofikia 100 mmHg au zaidi.

Hata hivyo, ni vizuri vipimo hivi vikatafsiriwa na daktari wako kuliko wewe mwenyewe. Na vipimo hivi vyote ni muhimu, bila ya kujali sistoliki au diastoliki.

Hata hivyo, umri ukifikia miaka 60, kipimo cha  sistoliki ndio kinakuwa muhimu zaidi. Kuna wakati mwingine ambapo kipimo cha diastoliki kinakuwa cha kawaida lakini hapohapo kipimo cha sistoliki kinakuwa juu, na hali hii inajitokeza zaidi kwa watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 60 na kuendelea.

 

Vitu vinavyochangia presha ya kupanda 

Uwezekano wa kupata presha unaongezeka kadri umri unavyoongezeka. Wataalamu wa magonjwa wanasema ni ngumu kuweza kufahamu sababu hasa inayosababisha presha.

Hata hivyo, kuna watu walio kwenye hatari ya kupata presha kama vile: Wenye uzito mkubwa; wenye ndugu wenye tatizo la presha; watu weusi na watu wa Caribbean; watumiaji wa chumvi kupita kiasi; wasiokula matunda na mboga za majani; wasiofanya mazoezi ya kutosha; wanywao kahawa kwa wingi au vinywaji vingine vyenye caffeine; wanywaji pombe kupita kiasi; wenye umri mkubwa zaidi ya 65.

Kama unaangukia katika moja ya hayo makundi,  unapaswa kubadilisha staili ya maisha yako ili kupunguza hatari ya kupata presha ya kupanda. Pia kuwa na tabia ya kupima presha ya damu yako angalau mara mbili kwa mwaka.

Makala hii imeandikwa na Benedict Kimbache

error: Content is protected !!