August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Fahamu Namba Zako’ kuhusu Shinikizo la Damu

Spread the love

KILA mwaka tarehe 17 Mei, Dunia huadhimisha Siku ya Shinikizo la Damu Duniani (WHD). WHD ilizinduliwa rasmi Mei 2005, tangu hapo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka.

Lengo kuu la WHD ni kuhamasisha na kuleta uelewa wa tatizo la shinikizo la damu kwa jamii, lakini pia lengo ni kuhimiza na kushawishi wananchi wa mataifa mbalimbali duniani kudhibiti na kuzuia ugonjwa huu unaoua kimyakimya na ambao umepewa jina la  ‘ugonjwa mlipuko wa kileo’ (modern epidemic).

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Fahamu Namba Zako’ (Know Your Numbers), kaulimbiu yenye lengo la kuongeza ufahamu wa tatizo hili kwa jamii mzima popote duniani.

‘Fahamu Namba Yako’ ni wito unaotolewa kwa kila mtu ili kuweza kuelewa shinikizo la damu kwamba linasoma namba zipi.

Kupata ufahamu wa vipimo vya shinikizo la damu/presha na madaraja yale kunayoweza kumpa mtu picha halisi ya Namba Zako soma hapa, makala iliyoandikwa na gazeti letu la mtandao. Vile vile ili uweze kufahamu athari za shinikizo la damu soma hapa.

Kwa mujibu wa Dk. Reuben Mutagaywa, bingwa wa magonjwa ya moyo wa Kikwete Cardiac Institute (JKCI), katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akiongea kuhusu siku hii kupitia Clouds TV leo amesema, takwimu zinaonesha katika kila Watanzania 100, 28 wana tatizo la shinikizo la damu.

Na kwamba, tatizo kubwa ni watu kufahamu kama wana tatizo hili. Katika asilimia 28 ya wagonjwa, ni asimilia 20 tu ndio wanaoelewa kuwa wana tatizo la shinikizo la damu.

Pamoja na 20% kujitambua kuwa na tatizo hili ni 10% tu wapo kwenye matibabu, matibabu ambayo yanafaidisha au yanadhibiti tatizo hili kwa 10% ya waliotibiwa.

Kutokana na uelewa mdogo wa tatizo hili, imetengwa siku maalum kuanzia tarehe 7 Mei 7 mpaka Mei 24 mwaka huu, wakati Tanzania ikiungana na dunia, inafanya kampeni ya kuelimisha jamii kuhsu ugonjwa huo kwa kuwataka wananchi kujitokeza na kwenda kupima katika vituo vya afya au JKCI.

Inasisitizwa kuwa ni vizuri kupima walau mara moja kwa mwaka kwa watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea,  kama mfumo wa maisha wa muhusika sio hatarishi, na kama ni hatarishi basi inashauriwa kupima zaidi ya mara moja kwa mwaka kadri itakavyoshauriwa na watalamu wa afya.

Maisha hatarishi hapa ni wale wote wenye uwezekano wa kupata shinikizo la damu kwa sababu ya uzito uliopita kiwango, matumizi ya sigara, matumizi ya pombe, kutofanya mazoezi, ulaji wa vyakula vyenye mafuta.

Kubwa zaidi linalosisitizwa ni ulaji wa vyakula visivyo na mafuta, upunguzaji wa kiwango cha chumvi kwenye chakula.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) chakula chenye kiwango kikubwa cha chumvi kinaua takribani watu milioni 3 duniani.

Zaidi ya watu milioni 300 wanakisiwa kuwa na shinikizo la damu lililotokana na ulaji wa chumvi uliopitiliza, hivyo inapendekezwa kwa mtu mzima kutumia chumvi isiyozidi gramu 5 (miligramu 2,000) kwa siku, uzito huu unaweza kufananishwa na uzito wa vidonge 10 vya Panadoli/Parasetamo.

Wakati tunaadhimisha Siku ya Shinikizo la Damu Duniani, serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuwa na utaratibu na mkakati wa kuhakikisha sehemu zinazotoa hudumaa ya afya, zinashiriki zoezi hili kikamilifu na kuwataka wananchi kupima afya zao na kujua ‘Namba zao’ za Shinikizo la Damu, lakini pia tunaisihi jamii mzima ya watanzania kuona umuhimu huo na kushiriki kikamilifu.

error: Content is protected !!