AFISA Usajili wa Biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Gift Raphael, amesema wafanyabishara na wawekezaji wanaotumia jina ya biashara wanaweza kulifunga jina hilo kisha kulitumia kufungua kampuni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Gift ameeleza mchakato huo leo kupitia Brela Online TV kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kufunga jina la kampuni na kutumia jina hilo kufungua kampuni.
“Cha kwanza unatakiwa ufunge jina la biashara na hii inatokana mara nyingi mtu anakuwa tayari amelitumia lile jina la bisahra na watu wameshamfahamu kwahiyo anataka alitumie jina hilo kwenye kampuni,” amesema
Amesema unachotakiwa kufanya wakati wa kufunga jina la biashara ni kujaza fomu namba saba ya kufunga jina la biashara inayopatikana katika tovuti ya BRELA.
Amesema taarifa za kujaza katika fomu hiyo ni pamoja na jina la biashara, namba ya usajili wa jina la biashara, lini umeacha kutumia hilo jina na lini umetoa taarifa ya kufunga jina la biashara, pamoja na jina na sahihi ya aliyesajili.
Amesema baada ya hapo mfanyabishara ataingia katika akaunti yake ambayo aliitumia kufungua jina la biashara.
“Hakikisha kwamba wakati unasajili jina la biashara mmiliki ndiye anajipa uwezo wa kufanya mabadiliko yeyote ikiwemo kufunga jina la biashara,” amesema Gift.
Amesema ukishaingia kwenye mfumo utachagua kufunga jina la biashara ambapo ataulizwa taarifa chache ikiwemo sababu ya kufunga jina la biashara.
“Hapa utaandika nataka kutoka kutumia jina la biashara na sasa litumike katika kampuni yangu kwasababu nimeshawekeza kwenye hilo jina,” amesema.
Amesema ukishajaza utapakua fomu ambayo inaitwa fomu yamajumuisho (Consolidated Form) na kuweka jina na saini yako kisha utaambatanisha na fomu namba tatu kisha kuziweka kwenye mfumo na kulipia kiasi cha Sh 15,000.
Gift amesema mchkato wa kufunga unakamilika ndani ya siku tatu za kazi ikiwa maombi hayo hayana dosari yeyote.
Amesema baada ya kufunga mfanyabisahara anaweza kuanza kusajili kampuni kwa jina lile aliloifunga kwa utaratibu wa kawaida.
Hata hivyo amesema anayetaka kutumia jina la baishara kwenye kusajili kampuni anatakiwa kueleza kwenye Katiba ya kampuni kuwa kampuni itachukua madeni na mali zote za jina la biashara aliyokuwa analitumia.
Amesema hii inasaidia kudhibiti ulipaji wa madeni na umiliki wa mali.
“Kama mtu alikuwa anadai jina la biashara ataendelea kudai kampuni yenye jina hilo” amesema Gift.
Amesema unaposajili kampuni kuna vitu mbalimbali ambavyo mfumo utakudai ikiwemo jina, eneo, wanahisa na taarifa zao.
Amesema kama wanahisa ni watanznaia wanatakiwa kuwa na namba za NIDA na endapo si watanzania wanapaswa kuwa na namba ya pasi ya kusafiria.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Wakurugenzi wa kampuni wanapaswa kuwa na namba ya mlipa kodi yaani TIN kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ameseam nyaraka zinazohitajika ni Katiba ya kampuni na nyaraka nyingine mbili zitapatikana kwenye mfumo ikiwemo fomu ya majumuisho na fomu ya maadili ambazo zitajazwa majina, sahihi na tarehe za kuweka sahihi hizo.
Leave a comment