January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Fahamu athari za Shinikizo la Damu

Mchoro wa Shinikizo la Damu

Spread the love

KUNA aina mbili za shinikizo la damu. Kwanza ni shinikizo la damu la juu (hypertension)  na pili ni shinikizo la damu la chini (hyportension). Makala hii itajadili aina ya kwanza.

Shinikizo la Damu la Juu ni hali ambayo msukumo wa damu unapokuwa  juu zaidi ya msukumo wa kawaida.

Shinikizo la damu la juu (maarufu kama presha ya kupanda) ni kipimo cha shinikizo la damu linalotokea kwenye kuta za mishipa ya damu ya ateri, moyo unaposukuma damu kuzunguka mwili.

Msukumo huu unakuwa mkubwa kuliko hali yake ya kawaida na ndiyo maana tunaita “shinikizo la damu la juu”.

Presha ya kupanda ikiwa kubwa kupita kiasi inasababisha tatizo kwenye mishipa ya damu, kwenye moyo, na baadaye inaweza  kupelekea tatizo la mshituko wa moyo (heart attack), kiharusi (stroke), figo kushindwa kufanya kazi vizuri (renal failure) n.k.

Changamoto ya ugonjwa huu ni kushindwa kujitambua kuwa unao. Unaweza kuwa na shinikizo la damu kwa miaka mingi bila  dalili yoyote kuonekana.

Hata hivyo, pamoja na kwamba unakuwa huna dalili, uharibifu wa mishipa ya damu na moyo  unaendelea na hapa ndipo dalili zinapoweza kuanza kuonekana.

Shinikizo la damu lisilodhibitiwa linaongeza hatari ya matatizo makubwa ya afya.

Shinikizo la damu la juu kwa kawaida ni kitu kinachojengeka kwa miaka mingi, na ni kitu kinachoathiri karibu nusu ya watu wenye umri kuanzia miaka 65 na kundelea.

Hata hivyo, habari njema ni kwamba tatizo la shinikizo la damu linagundulika kwa urahisi.

Ugonjwa huu wa msukumo wa damu unachangia vifo vingi vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza katika nchi za Jangwa la Sahara.

Watu wengi wana ugonjwa huu bila ya kujitambua, na ni ugonjwa ambao kama utaachwa bila ya tiba unaleta hatari ya kupata mshituko wa moyo (heart attack). Hii ni hali inayojitokeza moyo unaposhindwa kupata oksijeni ya kutosha au haupati oksijeni kwa kipindi fulani.

Katika jamii yetu tatizo la shinikizo la damu linazidi kuongezeka siku hadi siku.

Utafiti uliofanywa na Peck, R. na wenzake, uitwao “Hypertension – Related Diseases as common cause of hospital mortality in Tanzania: A 3 Year prospective study,” katika hospitali ya rufaa ya Bugando, Mwanza kati ya mwaka 2009 na 2011 umeonyesha kuwa shinikizo la damu lilichangia kwa asilimia 29.9 ya wagonjwa waliolazwa wenye matatizo yasiyoambukiza.

Utafiti huu pia uligundua kuwa kiharusi ni mojawapo ya matatizo yanayosababishwa na shinikizo la damu na kuongoza kwa vifo kwa wagonjwa wenye umri wa miaka 50.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Bugando, magonjwa kama HIV, Malaria na Kifua Kikuu, ni magonjwa ambayo kihistoria ndiyo yanayoongoza kwa wingi wa wagonjwa wanaolazwa mahospitalini na kuongoza kwa vifo.

Kati ya vifo 2,049 vilivyotokea kuanzia 2009-2011, vifo 927 sawa na asilimia 45.2 vilisababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Magonjwa mawili yaliyoongoza kwa vifo 927 yalikuwa HIV (vifo 684) na presha ya kupanda (vifo 314).

Presha ya kupanda unafahamika kama ugonjwa unaoua taratibu, kwani  si mara zote tatizo hili linakuwa na dalili za wazi na hivyo kufanya wengi wasijitambue kama wana tatizo hili.

Utafiti uliofanyika huko Uingereza, umeonyesha kuwa asilimia 30 ya wakazi wana presha ya kupanda bila ya kujitambua, na tatizo hili likiendelea kuachiwa bila ya kutibiwa, linapelekea kuongeza hatari ya kupata mshituko wa moyo au kiharusi.

 

Ushauri

Ili kuondoa tatizo lililojificha inashauriwa kuwa na tabia ya kuangalia afya kwa kupima presha. Inapendekezwa kuwa wenye umri mkubwa kuanzia miaka 50 wanapaswa kupima angalao mara mbili kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2000 asilimia 26.4 ya watu wazima walikuwa na presha ya kupanda.

Kati ya watu milioni 17 ya wagonjwa waliokufa kwa magonjwa ya moyo, watu milioni 9.4 ni kwa presha ya kupanda.

Presha ya kupanda, inasababisha asilimia 45 ya vifo kutokana na magonjwa ya moyo na pia asilimia 51 ya vifo kutokana na kiarusi.

Hii inaonyesha ni kwa kiwango gani presha ya kupanda ni changamoto kubwa katika jamii yetu. Sio tu mamlaka husika zinapaswa kuwajibika lakini wa kwanza ni watu wenyewe kwa kubadilisha mfumo wa maisha.

Mwandishi wa Makala haya ni Benedict Kimbache

error: Content is protected !!