March 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

EXIM benki yawafuata wasomi Udom

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)

Spread the love

TAASISI za kifedha zikiwamo benki zimetakiwa kupunguza riba katika mikopo yao ili kuwasaidia wananchi wanyonge, anaandika Dany Tibason

Ombi hilo limetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Christina Mndeme ambaye amesema kuwa riba katika mikopo imekuwa ni kikwazo cha kufanya mabenki yakimbiwe na wateja wao.

Mndeme alitoa kauli hiyo wakati akifungua tawi la benki ya Exim katika majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa koa wa Dodoma.

Amesema mikopo mingi inayotoewa na benki inakuwa na riba kubwa na jambo hilo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu, lakini hakuna anayeonyesha kujali.

“Serikali ya awamu ya tano inashughulika zaidi na wanyonge, nawaombeni mliangalie jambo hilo maana riba kubwa haziwasadii watu wa takaba la chini badala yake mnawaumiza zaidi,” amesema Mndeme

Akizungumzia utendaji katika tawi hilo, aliwataka watumishi wake kutanguliza weledi na kufanya kazi kwa ushindani na ubora huku akiwaomba Exim kuongeza matawi katika mji wa Dodoma ambao unakuwa kwa kasi.

Mkuu wa kitengo cha rasimilali watu wa Exim, Fredrick Kanga amesema tawi hilo limekamilisha ndoto ya muda mrefu kwa benki hiyo katika kuhamia Dodoma ambako ni makao makuu ya nchi.

Kanga amesema hilo ni tawi la 33 kwa benki hiyo ambayo imefungua matawi mengine nje ya nchi, lakini akabainisha kuwa watafanya kazi kwa ushindani mkubwa wa ubora katika eneo la Udom.

“Tunatambua zipo benki zingine, tutafanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuvutia zaidi wateja, tunatambua kuna wizara zaidi ya nane ambao ziko udom na idadi kubwa ya watumishi na wanafunzi, tumejipanga kuwahudumia,” amesema Kanga

Amesema Exim inaendelea kugawa ajira ambapo sasa imeajiri wafanyakazi 703 miongoni mwao ni 12 waliopangiwa kituo cha Dodoma na saba kati ya hao walichukuliwa Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Francisco Nzalalila amesema ujio wa benki hiyo utapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo ya foleni benki.

Profesa Nzalalila amesema Udom ina wanafunzi wengi na bado inaendelea kupokea zaidi na kwamba mwaka huu pekee wamepanga kupokea 10,000 hivyo huduma za benki ni muhimu.

error: Content is protected !!