January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

EWURA yashusha tena bei ya mafuta

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta, (EWURA), Felix Ngamlagosi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Spread the love

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa ambazo zitaanza kutumika kuanzia Machi 4, 2015. Anaandika Mwandishi wetu… (endelea).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, bei kikomo kwa rejereja kwa mkoa wa Dar es Salaam zitakuwa sh. 1,652 (petroli), 1,563 (dizeli) na 1,523 (mafuta ya taa) wakati bei kikomo za jumla ni sh. 1,547.19 (petroli), 1,457.58 (dizeli) na 1,547.19 (mafuta ya taa).

Ngamlagosi anasema bei za jumla na za rejareja kwa aina zote za mafuta, yaani, petroli, dizeli na mafuta ya Taa zimeshuka ikilinganishwa na bei katika toleo lililopita la Februari 4, 2015.

“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa viwango vifuatavyo: Petroli sh. 116/lita sawa na asilimia 6.57, Dizeli sh. 145/lita sawa na asilimia 8.49 na Mafuta ya Taa sh. 134/lita sawa na asilimia 8.08.,” amesema.

Aidha, kwa kulinganisha matoleo haya mawili, bei za jumla zimepungua kama ifuatavyo: Petroli, sh. 119.23/lita sawa na asilimia 7.16, Dizeli, sh. 147.94/lita sawa na asilimia 9.21, na Mafuta ya Taa, sh. 136.79/lita sawa na asilimia 8.80.

Kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la ndani kumetokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la Dunia.

Mkurugenzi huyo anaongeza kuwa, bei za mafuta masafi (refined petroleum products) katika soko la dunia, kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kati ya Julai 2014 na Januari 2015 kwa Dola 536/tani, Dola 400/tani na Dola 440/tani sawia sawa na punguzo la asilimia 53, 46 na 48 sawia.

“Kati ya Septemba 2014 na Machi 2015 bei za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa katika soko la ndani zimepungua kwa jumla ya kiasi cha sh. 615/lita, sh. 528/lita na Sh 517/lita sawia ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 27, 25 na 25, sawia,” amesema.

Katika kipindi husika, thamani ya shillingi ya Tanzania kulinganisha na dola ya Marekani ilishuka kwa asilimia 8. Bei ya mafuta kwenye soko la ndani ingeweza kupungua zaidi kama thamani ya shillingi isingeendelea kudhoofu.

Amesema kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 354 la tarehe 26 Septemba 2014.

error: Content is protected !!